Sep 10, 2018 10:42 UTC
  • Kuendelea siasa za chuki za Donald Trump dhidi ya Wapalestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema katika majibu yake kwa hatua ya Marekani ya kukata misaada yake kwa hospitali za Palestina huko Quds kuwa, hatua hiyo ni muendelezo wa njama zisizo na faida za Marekani za kuwatwisha Wapalestina mpango wa 'Muamala wa Karne'.

Akiendeleza siasa zake za chuki dhidi ya Wapalestina, Rais Donald Trump wa Marekani amekata misaada ya dola milioni 20 ya nchi hiyo ambayo ilitengwa kwa ajili ya hospitali za Palestina huko Quds. Aidha mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba, serikali ya Marekani ilisimamisha misaada yake yote kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira Kwa Ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Hivi karibuni Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Katika kipindi cha miaka 24 iliyopita, Marekani imewasaidia Wapalestina misaada yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 6. 

Uchunguzi kuhusiana na siasa za Marekani kuhusu Wapalestina katika kipindi hiki unaonyesha kuwa, Washington imekuwa ikitumia misaada hiyo kama wenzo wa kutaka upendeleo kutoka kwa Wapalestina sanjari na kusukuma mbele gurudumu la malengo ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira Kwa Ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Israel ni moja ya madola yanayopata misaada mingi zaidi kutoka Marekani. Utawala haramu wa Israel umekuwa ukipokea misaada isiyo na masharti yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 3 kwa mwaka kutoka Marekani.  Licha ya Marekani kutoa misaada yote hiyo mingi kwa Wazayuni katika miongo kadhaa iliyopita, lakini imeamua kukata misaada ya Wapalestina ambayo si lolote si chochote ikilinganishwa na misaada yake kwa Wazayuni maghasibu.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana wakosoaji wa serikali ya Washington wanasema kuwa, siasa hizo za White House lengo lake ni kuwatwisha Wapalestina mwenendo wa mapatano na Wazayuni. Uamuzi wa Marekani wa kuwakatia misaada Wapalestina unakinzana na madai yake ya kutoa misaada kwa ajili ya kuimarisha amani na utulivu katika Mashariki ya Kati hasa kwa kutilia maanani kwamba, hatua hiyo ni madhara kwa Wapalestina.

Mtandao mmoja wa habari wa Kifaransa umeripoti juu ya kutekelezwa kimya kimya mpango eti wa mapatano wa 'Muamala wa Karne' na kueleza kwamba, lengo lake ni kuifutilia mbali kadhia ya Palestina.

Uhaba wa maji ni moja ya matatizo yanayowakabili wananchi wa Ukanda wa Gaza

Mtandao huo wa Mediapart umeandika katika uchambuzi wake kwamba: Licha ya Donald Trump kuchelewa kutangaza rasmi mpango wenye utata wa 'Muamala wa Karne', lakini kivitendo serikali ya Marekani imeanza kutekeleza baadhi ya vipengee vya mpango huo kupitia kuhamishia ubalozi wake mjini Beitul-Muqaddas na kukata misaada yake kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira Kwa Ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA). 

Kwa mujibu wa Mediapart ni kuwa: ilipangwa kuwa, Jared Kushner mkwe wa Donald Trump na mshauri wake mkuu pamoja na Jason Greenblatt mwakilishi maalumu wa Trump wautangaze mpango wa 'Muamala wa Karne' wa kurasa 40 mwanzoni mwa  mwezi huu, hata hivyo hilo halikufanyika. Hii ni katika hali ambayo, kivitendo utekelezwaji wa mpango huo uumeshaanza.

Marekani ikiwa na lengo la kusukuma mbele mpango huo, haijaacha kutekeleza hatua yoyote ile isiyo ya kibinadamu wala inayokinzana na kimaadili. Serikali ya Washington iko tayari hata kutumia vibaya mazingira magumu ya maisha wanayokabiliwa nayo wagonjwa huko Palestina ili tu ifanikiwe kutekeleza mpango wake wa 'Muamala wa Karne'.

Maandamano ya kupinga mpango wa 'Muamala wa Karne'

Siasa za uhasama za Marekani dhidi ya Wapalestina zinaonyesha adawa na chuki ya hali ya juu walionayo viongozi wa Washington ambapo wakiwa na nia ya kufikia malengo yao hawajali wala kuheshimu maadili, utu au sheria za kimataifa. Ukweli ni kuwa, Marekani imekuwa pamoja na Israel katika jinai zake dhidi ya Wapalestina.

Jambo hilo linaonyesha kuwa, harakati za Marekani dhidi ya Wapalestina zimeingia katika marhala na hatua hatari zaidi. Katika mazingira haya, walimwengu wanashuhudia kufikia kilele cha juu kabisa hatua za kukiuka maadili za serikali ya Marekani katika kipindi cha uongozi wa Donald Trump, ambapo kufanya njama, mauaji, ukandamizaji, kuyawekea vikwazo mataifa mengine, ushari na kukiuka haki za mataifa mengine ni mambo ambayo yamewekwa katika ajenda za serikali ya sasa ya Washington.

Maoni