Sep 11, 2018 04:16 UTC
  • Kurudi nyumbani wakimbizi wa Syria; kurejea katika maisha yao

Zaidi ya wakimbizi 255,000 wa Syria waliokuwa wamekimbilia nchini Uturuki wamerejea nyumbani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mgogoro wa kutwishwa Syria ulianza Machi 2011. Baada ya kupita muda tangu kuanza mgogoro huo na kuingia nchini Syria magaidi waliokuwa wakiungwa mkono na baadhi ya nchi za Kiarabu, madola magharibi na Wazayuni, taratibu mwenendo wa wakimbizi wa nchi hiyo waliokuwa wakiimbia nchi yao kutokana na machafuko nao ukawa ukiongezeka na kuifanya idadi ya raia wa nchi hiyo kupungua siku baada ya siku.

Wakati mgogoro wa Syria unaibuka nchi hiyo ilikuwa na wakazi zaidi ya milioni 23.5. Hata hivyo vita vilivyoanzishwa na magaidi na kuharibiwa nyumba hali iliyoyafanya maisha ya wananchi kuwa magumu, kulisababisha Wasyria zaidi ya milioni 12 wayakimbie makazi yao na kuwa wakimbizi.

Rais Bashar al-Assad wa Syria

Takribani Wasyria milioni 6 wamekimbilia nje ya nchi huku nusu ya waliobakia wakiwa wakimbizi ndani ya nchi yao. Kati ya wakimbizi milioni 6 wa Syria waliokimbilia nje ya nchi, milioni 2.5 hadi milioni 3 walikimbilia Uturuki, milioni 1.2 nchini Lebanon, zaidi ya 660,000 waliomba hifadhi nchini Jordan na takribani milioni moja walikimbilia katika nchi za Ulaya.

Katika kipindi cha miaka 7 iliyopita, wakimbizi wa Syria wamepitia kipindi kigumu mno cha mazingira mabaya ya maisha. Idadi kubwa ya wakimbizi hao walikufa hata kabla ya kufika katika nchi walizokusudia kukimbilia na wengine wakiaga dunia baada ya kuwasili huko.

Aidha akthari ya wakimbizi wa Syria walilazimika kuishi katika kambi za wakimbizi za nchi nyingine, kambi ambazo hazikuwa hata na huduma na suhula za awali kabisa kwa ajili ya maisha ya mwanadamu.

Wakimbizi wa Syria

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza katika ripoti yake kwamba, zaidi ya asilimia 93 ya wakimbizi wa Syria waliokimbilia nchini Jordan wanaishi chini ya mstari wa umasikini.

Kutazamwa kwa jicho lenye maana maalumu na raia wa nchi walizokimbilia wakimbizi wa Syria, ni jambo ambalo nalo limewasababishia wakimbizi hao matatizo makubwa ya kinafsi. Fauka ya hayo watoto wakimbizi wa Kisyria wamekosa kabisa fursa ya kwenda shule. Kadhalika idadi ya wanawake na mabinti wakimbizi wa Kisyria waliokumbwa na masaibu ya kubakwa nayo si ndogo.

Hali ya wakimbizi wa Syria nje ya nchi ni mbaya mno kisiasa kwamba, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, asilimia 90 ya wakimbizi hao walioko Lebanon, Uturuki na Jordan wanataka kurejea nchini kwao.

Ushindi mtawalia lilioupata jeshi la Syria na waitifaki wake katika kipindi cha miaka miwili iliyopita katika vita dhidi ya ugaidi umehuisha matumaini ya kurejea wakimbizi wa Kisyria katika nchi yao.

Wanajeshi wa Syria wakishangilia baada ya kukomboa moja ya miji iliyokuwa ikidhibitiwa na magaidi

Mwezi uliopita, serikali ya Russia ilipendekeza mpango wa kurejea wakimbizi wa Syria hatua kwa hatua. Katika hatua ya awali ya mpango huo, wakimbizi 890,000 wa Syria walioko nchini Lebanon wanatarajiwa kurejea nchini kwao.

Gazeti mashuhuri la al-Sharq al-Awsat limezinukuu duru rasmi za Lebanon na kutangaza kuwa, kuanzia Julai 23 hadi Agosti 23 mwaka huu kulirekodiwa idadi ya Wasyria 16,000 waliotaka kurejea kwao kwa hiari. Hii ni katika hali ambayo, hadi sasa zaidi ya wakimbizi laki mbili na nusu wa Kisyria waliokuwa nchini Uturuki wamerejea nchini Syria.

Licha ya kuwa serikali ya Syria imeandaa mazingira ya kurejea wakimbizi wa nchi hiyo baada ya kukombolewa miji iliyokuwa chini ya uudhibiti wa makundi ya kigaidi, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, wakimbizi hao ili warejee katika maisha yao ya kawaida, wanahitajia misaada ya kibinadamu ya asasi za kimataifa na mataifa mbalimbali ya dunia.

Maoni