Sep 11, 2018 04:17 UTC
  •  Indhari ya nchi tano za Ulaya kwa utawala wa Kizayuni wa Israel

Nchi tano za Ulaya zimeutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya utawala huo kuchukua uamuzi wa kubomoa kijiji cha Khan al Ahmar mashariki mwa mji mtakatifu wa Quds.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imeeleza kuwa nchi hiyo pamoja na Ufaransa, Ujerumani, Uhispania na Italia zinatiwa wasiwasi na uamuzi huo wa utawala wa Kizayuni wa kutaka kubomoa kijiji cha Khan al Ahmar huko Quds na kusistiza kuwa hatua hiyo itakuwa na taathira kubwa. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imefafanua kuwa kijiji cha Khan al Ahmar kina umuhimu wa kistratejia kwa ajili ya kulinda umoja wa serikali ijayo ya Palestina. 

Wapalestina na wanaharakati wakizuia kubomolewa kijiji cha Khan al Ahmar

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imeashiria dikrii iliyotolewa Jumatano iliyopita na mahakama ya utawala wa Kizayuni wa Israel iliyoamuru kubomolewa na kufukuzwa wakazi wa kijiji hicho na kueleza kuwa: Inaitaka Israel iachane na uamuzi huo kwa sababu hatua hiyo itapelekea kubomolewa shule na kuwafanya wakazi wa kijiji hicho kuwa wakimbizi.

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na wanaharakati wanaotetea haki za Wapalestina wamelaani uamuzi huo wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kutaka kubomoa kijiji hicho na kusema kuwa hatua ya aina hiyo ni kikwazo kipya katika uundaji wa nchi huru ya Palestina. 

Tags

Maoni