Sep 11, 2018 04:45 UTC
  • Serikali ya Saudia yampandisha kizimbani mwendesha vipindi wa TV kwa kuiunga mkono Ikhwanul Muslimin

Mahakama ya Jinai nchini Saudia imemsomea mashitaka mwendesha vipindi wa televisheni ya nchi hiyo kwa tuhuma za kuiunga mkono harakati ya Ikhwanul Muslimin.

Mtandao wa habari wa gazeti la kielektroniki la Sabq, wa nchini Saudia umeandika kuwa, miongoni mwa tuhuma zinazomkabili mwendesha vipindi huyo wa televisheni na ambaye jina lake halikuwekwa wazi ni, kujihusisha na hatua za uchochezi, kuunga mkono harakati za kupigania uhuru katika nchi kadhaa za Kiarabu na kuunga mkono harakati za wananchi nchini humo. Hata hivyo gazeti hilo la Sabq halikufafanua zaidi ni muda gani mtuhumiwa huyo alipandishwa kizambani katika mahakama za Saudi Arabia.

Chuki ya kupindukia ya Saudia dhidi ya Harakati ya Ikhwanul Muslimin

Katika wiki za hivi karibuni, mahakama za Saudia ziliwasomea mashitaka Salman al-Ouda na Ali al-Amri, ambao ni viongzo wa kidini wa nchi hiyo kwa tuhuma za uungaji mkono kwa harakati ya Ikhwanul Muslimin na ugaidi. Aidha mwezi uliopita Wizara ya Habari ya Saudia ilitoa taarifa ya kupiga marufuku, kuingiza, kuchapisha, kugawa na kuweka katika maktaba za nchi hiyo vitabu vinavyohusiana na harakati ya Ikhwanul Muslimin. Serikali ya Saudia inaitambua harakati hiyo kuwa moja ya makundi ya kigaidi sawa na kundi la al-Qaidah na Daesh. Mwezi Novemba mwaka jana, Mohammad bin Salman bin Abdulaziz Al Saud, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia akizungumza na gazeti la Time la nchini Marekani alidai kwamba, Ikhwanul Muslimin ni kundi hatari zaidi kuliko makundi yote ya dunia katika kipindi cha miaka 100 ya hivi karibuni.

Sheikh Salman al-Ouda mmoja wa masheikh waliopandishwa kizimbani Saudia hivi karibuni

Inafaa kuashiria kuwa, harakati ya Ikhwanul Muslimin ni mrengo wa Kiislamu wa Kisuni ambao umeenea katika nchi nyingi za Kiarabu huku ukiwa na wafuasi wengi na hivyo kuhesabiwa kuwa unaoweza kuwa moja ya makundi makubwa ya kisiasa duniani ya Waislamu wa Suni. Mwaka 1928 Miladia harakati hiyo ilianzishwa katika mkoa wa Ismailia nchini Misri chini ya uongozi wa Hassan al-Banna na kisha kuenea katika nchi nyingine za Kiarabu na Kiislamuu. Msingi wa harakati hiyo ni kukosoa uingiliaji wa madola ya kigeni katika nchi za Kiislamu.

Tags

Maoni