Sep 11, 2018 07:08 UTC
  • Jinai ya kimasomo ya utawala wa Aal-Saud dhidi ya watoto wa Yemen na Syria

Wizara ya Elimu na Malezi ya Saudi Arabia imezitaka shule za serikali ya nchi hiyo kuzuia usajili wa watoto wa Yemen na Syria kusoma katika shule hizo.

Asilimia 38 ya jamii ya watu milioni 32.5 ya Saudi Arabia, inaundwa na raia wa nchi nyingine zikiwemo Syria na Yemen. Raia hao wa Syria na Yemen hawakuhamia nchini Saudia katika miaka ya hivi karibuni, bali walikimbilia nchi hiyo miongo mingi iliyopita. Baada ya kuibuka mgogoro wa Syria hapo mwaka 2011 na uvamizi wa Saudia nchini Yemen hapo mwezi Machi mwaka 2015, utawala wa Aal-Saud, ulianzisha mashinikizo makubwa dhidi ya raia wa nchi hizo mbili wanaoishi nchi hiyo, kutokana na uhasama ulionao kwa serikali za Damascus na Sanaa. Katika uwanja huo, miongoni mwa machaguo muhimu ambayo yamekuwa kwenye meza ya serikali ya Riyadh, ni kuwafukuza raia wa Yemen na Syria nchini humo.

Kitendo cha Saudia kuwanyima elimu watoto wa Yemen na Syria, ni sawa na kitendo cha Israel kuwanyima elimu watoto wa Palestina

Ukweli ni kwamba, uhasama wa utawala wa Aal Saud dhidi ya Syria na Yemen haukuishia tu kwa serikali za nchi hizo, bali umevuka mpaka hadi kwa raia wake wanaoishi nchini Saudia. Moja ya uhasama wa Aal-Saud dhidi ya raia wa Yemen na Syria wanaoishi nchi hiyo ni kuwazuia watoto wao kusoma. Hii ni baada ya serikali ya Saudia kuzitaka shule za nchi hiyo kuacha kuwaandikisha watoto wa nchi mbili hizo katika shule zake. Baada ya amri hiyo kukabiliwa na radiamali kali, serikali ya Riyadh sambamba na kurejea nyuma kuhusiana na uamuzi wake huo, imetangaza kwamba, itawaruhusu kusoma watoto ambao tayari walikuwa wamejiandikisha katika shule za serikali miaka kadhaa iliyopita, huku ikiwazuia wale ambao wanajiandikisha kwa mara ya kwanza. Kwa hakika jinai hazikomei tu kwenye kuua na kuwajeruhi wanadamu, bali wakati serikali ya nchi fulani inapowanyima watoto wadogo haki yao ya kusoma na kutafuta elimu, hiyo huwa ni jinai  mbaya zaidi kuliko hata ya kuua na kujeruhi. Hii ni kwa kuwa kuwanyima watoto elimu ni kuharibu mustakbali wao na kuwadhuru kisaikolojia moja kwa moja.

Watoto wa Yemen na Syria hawaruhusiwi kusoma Saudia

Serikali ya Saudia inakataa kuwaandikisha watoto wa Yemen na Syria katika shule zake katika hali ambayo, hati ya haki ya watoto iliyopitishwa mwaka 1989, inaitambua elimu kuwa haki yao ya msingi na kwamba kuwasomesha bure, ni jukumu la serikali zote. Kipengee cha 28 cha hati hiyo ya haki ya watoto kinasisitiza kwamba, nchi zilizoitia saini ni lazima ziandae mazingira ya kuwawezesha watoto kupata elimu, kuwasomesha bure, kuwashawishi kwenda shule na kutokomeza ujinga kati yao. Jinai za Saudi Arabia dhidi ya watoto wa Syria na Yemen zinatekelezwa katika hali ambayo ndege za kivita za nchi hiyo bado zinaendelea kufanya mauaji ya kutisha dhidi ya watoto wa Yemen, ambapo mfano wa wazi wa mauaji hayo ni shambulizi la jinai lililotekelezwa tarehe tisa mwezi jana ambapo zaidi ya watoto 120 wa shule ya Qur'ani waliuawa na kujeruhiwa kikatili na ndege za utawala wa Aal-Saud nchini Yemen.

Maoni