Sep 11, 2018 07:12 UTC
  • Uturuki yapinga kuangamizwa magaidi mkoani Idlib, Syria

Sambamba na jeshi la Syria kujiandaa kwa mashambulio ya kuiangamiza ngome kuu ya makundi ya kigaidi katika mkoa wa Idlib kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, Uturuki imetangaza msimamo wa kupinga hatua hiyo.

Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Jenerali Hulusi Akar amesema: mashambulio ya angani na ardhini ya jeshi la Syria katika mkoa wa Idlib yanapasa kusitishwa. Pasi na kuashiria madhara ya kuendelea harakati za magaidi mkoani Idlib na katika maeneo mengine ya Syria, Akar amedai kuwa operesheni dhidi ya magaidi huko Idlib zitasababisha maafa ya roho za watu.

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki naye pia alitangaza hapo jana kuwa shambulio ambalo jeshi la Syria limepanga kufanya Idlib na kutimuliwa makundi ya kigaidi na ukufurishaji katika mkoa huo ni jambo lenye kutia wasiwasi.

Mkoa wa Idlib ungali unadhibitiwa na wanamgambo wa upinzani pamoja na makundi ya kigaidi; na serikali ya Syria inataka kuukomboa mkoa huo kutoka kwenye makucha ya magaidi yanayoungwa mkono na baadhi ya nchi za eneo na za Magharibi.

Kufuatia ushindi liliopata jeshi la Syria katika kipindi cha mwaka mmoja sasa, idadi kubwa ya wapinzani wa serikali ya Damascus pamoja na familia zao wamekimbilia eneo la Idlib na inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni tatu wako kwenye mji huo na maeneo ya kandokando yake.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo ni mmoja wa waitifaki wa serikali ya Syria inataka kadhia ya Idlib itatuliwe kwa njia za kisiasa na kuhakikisha maafa ya kibinadamu yanakuwa ya kiwango cha chini kabisa.../

Tags

Maoni