Sep 12, 2018 01:18 UTC
  • Radiamali ya Wapalestina kwa uamuzi wa Marekani wa kufunga ofisi ya PLO mjini Washington

Husam Badran, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa, uamuzi wa serikali ya Marekani wa kufunga ofisi ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO mjini Washington inabainisha kutokuwa na matunda mwenendo wa mapatano.

John Bolton, mshauri wa usalama wa taifa wa rais wa Marekani alitangaza rasmi Jumatatu iliyopita uamuzi wa kufungwa ofisi ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO mjini Washington. Akitangaza uamuzi huo Bolton alisema, ofisi ya PLO mjini Washington inafungwa na kwamba, haitafunguliwa madhali Wapalestina hawajakaa katika meza moja ya mazungumzo na Israel. Uamuzi wa Marekani wa kufunga ofisi ya PLO mjini Washington na kupinga uchunguzi wowote ule kuhusu jinai za utawala dhalimu wa Israel ni mambo yanayofanyika katika fremu ya siasa zilizo dhidi ya Palestina zinazotekelezwa na rais wa nchi hiyo Donald Trump.

Siasa hizo zimepelekea kuhamishiwa ubalozi wa Marekani mjini Quds, kutambuliwa mji huo kama mji mkuu wa utawala bandia wa Israel na kukatwa misaada ya Washington kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira Kwa Ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

John Bolton, mshauri wa usalama wa taifa wa wa rais wa Marekani

Uamuzi wa Marekani wa kufunga ofisi ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO mjini Wshington lengo lake ni kupanua wigo wa mashinikizo dhidi ya Wapalestina katika uga wa kidiplomasia na hivyo kuwafanya Wapalestina waachane na muqawama wowote ule mbele ya mpango wenye njama wa 'Muamala wa Karne' sambamba na kuwafanya waache kufuatilia jinai za Israel katika uga wa kimataifa.

Lengo jingine la hatua hizo za Marekani ni kuwashinikiza Wapalestina ili warejee tena katika meza ya mazungumzo eti ya mapatano na kuzidi kuzinyakua haki zao kadiri inavyowezekana kupitia mpango unaojulikana kama 'Muamala wa Karne'. 

Jean-Baptiste Fallevoz, mtaalamu wa masuala ya kimataifa wa Kanali ya Televisheni ya France-24 anasema: Hatua ya Rais Donald Trump ya kufunga ofisi ya Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO mjini Washington na vile vile  kukata misaada yake kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira Kwa Ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) ni kutaka kuwavuta Wapalestina katika meza ya mazungumzo. Ukweli wa mambo ni kuwa, tangu Marekani iitambue Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, Wapalestina hawana hamu kabisa ya kufanya mazungumzo na Trump pamoja na serikali yake. Wapalestina walimpuuza hata Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani wakati alipofanya safari ya kiduru Mashariki ya Kati na hata wakawasilisha kesi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Ofisi ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) mjini Washington

Matukio ya Palestina na kufungwa ofisi za PLO nchini Marekani yanabainisha kuwa, viongozi wa Washington hawako tayari kustahamili harakati ya aina yoyote ile ya Wapalestina hata katika kiwango cha Mamlakka ya Ndani ya Palestina. Hatua ya Marekani ya kufunga ofisi ya PLO ni ishara ya kugonga mwamba kikamilifu mwenendo wa mapatano. Aidha hatua hiyo inaweka wazi ukweli huu kwamba, Wapalestina hawawezi kufikia malengo yao matukufu kupitia mwenendo wa mapatano, bali njia pekee ya kufikia hilo ni muqawama na mapambano.

Ni kwa kutegemea muqawama huo, ndio maana katika miaka ya hivi karibuni, walimwengu wameshuhudia kuimarika nafasi ya Wapalestina katika Umoja wa Mataifa na kupata uanachama katika asasi mbalimbali za umoja huo ikiwemo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC na hivyo kuandaa uwanja na uwezekano wa kuweza kuwasilisha mashtaka ya jinai za Israel katika uga wa kimataifa.

Rais Donald Trump wa Marekani

Kupanuka wigo wa uwakilishi wa Palestina katika maeneo mbalimbali duniani ambapo kwa sasa Palestina ina wawakilishi zaidi ya 100 katika nchi tofauti ulimwenguni mwenendo ambao umekuwa ukiongezeka siku baada ya siku, yanahesabiwa kuwa matunda na mafanikio ya muqawama wa wananchi wa Palestina katika uga wa kidiplomasia katika miongo kadhaa sasa hususan katika miaka ya hivi karibuni.

Katika mazingira kama haya, kutazama upya Mamlaka ya Ndani ya Palestina mwenendo wa mapatano na Israel na wakati huo huo kuwa pamoja na muqawama wa Palestina sambamba na kuimarisha misimamo ya Wapalestina katika kukwamisha njama za Marekani hususan 'Muamala wa Karne' itaandaa uwanja wa kufikiwa malengo matukufu ya Wapalestina mhimili mkuu ukiwa ni kuundwa nchi huru ya Palestina, mji mkuu wake ukiwa Beitul-Muqaddas. 

Tags

Maoni