Sep 12, 2018 07:01 UTC
  • Kulaaniwa jinai za Saudi Arabia nchini Yemen na Waziri wa Haki za Binadamu wa Pakistan

Waziri wa Haki za Binadamu wa Pakistan amelaani mauaji ya kizazi ya Saudi Arabia dhidi ya wananchi madhulumu wa Yemen.

Shireen Mazari amebainisha kwamba, Saudi Arabia imekiuka na kukanyaga haki za binadamu mara chungu nzima nchini Yemen kutokana na kufanya mashambulio ya kikatili dhidi ya  wananchi wa nchi hiyo wakiwemo wanawake na watoto wadogo.

Waziri wa Haki za Binadamu wa Pakistan amesema kuwa, kuuawa makumi ya watoto wa shule baada ya Saudi Arabia kushambulia basi lililokuwa limewabeba watoto hao al-Dhahyan kwa hakika lilikuwa tukio chungu na la kuumiza moyo mno na kuongeza kuwa, utawala wa Aal Saud unapaswa kusitisha mashambulio yake huko Yemen.

Bi Shireen Mazari amezitaka nchi za Kiislamu kutatua matatizo na hitilafu zao kupitia Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na sio kupitia kwa Marekani na madola ya Magharibi na kujiepusha na umwagaji damu na mauaji katika ardhi za Kiislamu.

Mfalme Salman bin Abdul Aziz wa Saudi Arabia ambaye nchi yake inaendelea kuua raia wa Yemen

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi za juu wa serikali na wa chama nchini Pakistan kulaani jinai za Saudi Arabia nchini Yemen na kuzitaja kuwa ni mauaji ya kizazi.

Hii ni ishara kwamba, serikali ya Imran Khan Waziri Mkuu mpya wa Pakistan imo katika hatua za kutazama upya ushirikiano wake na Riyadh katika vita vya Aal Saud dhidi ya wananchi madhulumu wa Yemen. Aidha inaonekana kuwa, serikali ya Imran Khan nyota wa zamani wa mchezo wa kriketi imo mbioni kusaidia juhudi za kupatikana umoja na ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu.

Katika kipindi cha utawala wa Chama cha Muslim League nchini Pakistan cha Waziri Mkuu Muhammad Navaz Sharif, licha ya kuwa serikali yake ikiathiriwa na miswada iliyokuwa ikipasishwa na Bunge ilijizuia kushirikiana moja kwa moja na kwa dhahiri na Saudi Arabia katika vita dhidi ya wananchi wa Yemen, lakini ushirikiano wa Raheel Sharif mkuu wa zamani wa jeshi la Pakistan na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia katika vita vya Yemen na hatua yake ya kutuma wanajeshi wa nchi hiyo huko Saudi Arabia kwa kile kilichokuwa kikielezwa kuwa, kwenda kupata mafunzo ya kijeshi, ni mambo yaliyodhirisha kwamba, licha ya upinzani wa wananchi na Bunge, serikali hiyo iliazimia kushirikiana na watawala wa Riyadh katika vita vyao dhidi ya Yemen.

Imran Khan Waziri Mkuu mpya wa Pakistan

Allamah Mubashir Hassan, mmoja wa viongozi wa Chama cha Wahdat-e-Muslimeen katika mji wa Karachi Pakistan anasema:

Saudi Arabia na washirika wake wamekuwa wakiwaua kinyama wanachi wasio na hatia wa Yemen kama wanavyouawa wananchi madhulumu wa Palestina. Saudi Arabia imekuwa ikishambulia kwa mabomu miji ya Sana'a, Saada na miji mingine ya  Yemen kama utawala wa Kizayuni wa Israel unavyoishambulia Gaza. Hivyo basi, kimya cha jamii ya kimataifa dhidi ya waenezaji wa vita, nayo inahesabiwa kuwa ni hiana na usaliti.

Kwa mtazamo wa duru za kisiasa nchini Pakistan ni kuwa, msimamo wa serikali mpya ya Islamabad kwa uongozi wa Waziri Mkuu Imran Khan dhidi ya Saudi Arabia unaongeza matumaini ya kusitishwa vitendo vya utumiaji mabavu na mauaji dhidi ya wananchi wa Yemen. 

Endapo Pakistan itachukua uamuzi kama wa Malaysia wa kusimamisha rasmi ushirikiano na utawala wa Aal Saud katika vita dhidi ya wananchi wa Yemen, hapana shaka kuwa, Riyadh itatengwa zaidi katika suala la kuendelea na mauaji huko Yemen.

Raia wengi wa Yemen wamekosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa na mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia

Vyovyote itakavyokuwa, kwa kuzingatia kuongezeka mashinikizo ya Marekani dhidi ya nchi za Kiislamu, kuweko umoja na mshikamano baina ya Waislamu ni jambo la dharura kuliko wakati mwingine wowote ule.

Misimamo mipya ya serikali ya Imran Khan ya kuwatetea Waislamu inazidi kuleta matumaini ya umoja na mshikamano zaidi katika Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kushirikiana dhidi ya dhulma na ukandamizaji unaofanywa na baadhi ya madola ya Kiarabu katika Mashariki ya Kati yakiongozwa na Saudi Arabia.

Tags

Maoni