Sep 12, 2018 07:45 UTC
  • Sisitizo la Ibrahim Jaafari la kuondoka wanajeshi wa Uturuki huko Iraq

Ibrahim Jaafari Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesisitiza kuondoka haraka iwezekanavyo wanajeshi wa Uturuki katika ardhi ya nchi hiyo.

Katika miaka ya hivi karibuni Uturuki imetekeleza mashambulizi kadhaa katika ardhi ya Iraq kwa kisingizio cha kuwakandamiza wapiganaji wa Kikurdi wa PKK wa Uturuki; mashambulizi ambayo yamekabiliwa na radiamali kali ya serikali ya Iraq na nchi nyingine. Akizungumza katika kikao cha baraza la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu( Arab League) huko Cairo Misri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amelaani msimamo wa Uturuki kutokana na mashambulizi ya wanajeshi wa nchi hiyo katika eneo la Bashiqa nchini Iraq na kueleza kuwa: Kuendelea kuwepo wanajeshi wa Uturuki katika ardhi ya Iraq ni jambo lisilokubalika.  

Al Jaafari ameongeza kuwa licha ya kwamba Arab League imelaani chokochoko hizo za Uturuki huko Iraq na kutaka kuondoka wanajeshi hao katika eneo la Bashiqa, lakini Uturuki ingali inaendelea na hatua yake hiyo. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq pia ameashiria hamu ya Baghdad ya kustawisha uhusiano na Ankara na kueleza kuwa Iraq haipingi kuwa na uhusiano na nchi yoyote jirani yake, lakini hiyo haimaanishi kunyamaza kimya mbele ya uchokozi na kukiukwa mamlaka ya kujitawala Iraq. 

Wanajeshi wa Uturuki waliopo katika mji wa Bashiqa kaskazini mwa Iraq 

 

 

Tags

Maoni