• UN yaelezea kusikitishwa na hali mbaya ya Ukanda wa Ghaza

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya maendeleo na biashara ametoa ripoti maalumu kuhusu maafa ya kibinadamu ya Ukanda wa Ghaza na kuongezeka kupindukia idadi ya Wapalestina wasio na kazi akisema kuwa hali hiyo inasikitisha sana.

Hayo yameelezwa na gazeti la al Hayat linalochapishwa mjini London Uingereza na kumnukuu Bi Isabelle Durant, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya maendeleo na biashara akisema jana Jumapili mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kuwa, kadiri siku zinavyopita ndivyo hali ya Ghaza inavyozidi kuwa mbaya na kwamba haiwezekani kuendelea kunyamazia kimya janga hilo kubwa la kibinadamu.

Ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel hauhurumii hata vitoto vichanga

 

Naibu Katibu Mkuu huyo wa UN katika Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo na Biashara UNCTAD aidha ameilaumu vikali Marekani kwa kukata michango yake iliyo wajibu kuitoa kwa ajili ya kuendeshea Wakala wa Umoja wa Mataifa wa Kazi na Misaada kwa Wakimbizi wa Palestina UNRWA na kusema kuwa, Israel inaendelea kuiwekea vikwazo vya kila upande Ghaza na jambo hilo limeongeza maradufu masaibu ya wananchi wa Palestina.

Kwa mujibu wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo na Biashara UNCTAD, ukosefu wa ajira katika ukanda huo unaifanya Ghaza kuwa eneo linaloongoza kwa idadi ya watu wanaoishi kwenye mazingira magumu sana duniani kutokana na kuongezeka ukosefu wa ajira kwa zaidi ya asilimia 27, huku pato la kila mtu likishuka, uzalishaji wa kilimo ukipungua kwa asilimia 11 na hali ya kiuchumi na kijamii kwa mwaka 2017 ikizidi kuzorota.

Tags

Sep 17, 2018 02:22 UTC
Maoni