Sep 18, 2018 03:56 UTC
  • Kutimuliwa Balozi wa Palestina nchini Markeani; hatua mpya ya Washington katika kuunga mkono Israel

Hatua za kiuadui za Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Palestina na kuunga mkono kwake utawala haramu wa Israel kwa namna isiyo na kifani sasa zimeingia katika duru mpya.

Marekani kama mshirika wa kistratijia wa Israel daima imekuwa ikizingatia uungaji mkono wa utawala huo kama nukta ya kimsingi ya sera zake za kigeni.

Katika uga huu, baada ya Marekani kukata misaada yake kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA),  mara hii imeamua kumtimua Balozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aliyeko Washington. Husam Zomlot, Balozi wa Palestina nchini Marekani ametangaza kuwa, wakuu wa Marekani wamemtaka aondoke nchini humo mara moja pamoja na kuwa vitambulisho vyake vilimruhusu awe balozi hadi mwaka 2020.

Wakuu wa Marekani wamebatilisha visa ya Zomlot na familia yake na kufunga akaunti zake zote za benki.

Hannan Ashrawi, mwanachama wa Kamati ya Utendaji katika Harakati ya Ukombozi wa Palestina, PLO,  amesema hatua hiyo ya Marekani ambayo imechukuliwa na utawala wa Trump ni ya ulipizaji kisasi . Amesema Marekani ina chuku dhidi ya uongozi pamoja na watoto na wanawake wa Palestina.

Mnamo Septemba 10,  Marekani ilitangaza rasmi kufunga ofisi ya uwakilishi wa kidiplomasia wa Palestina mjni Washington na kudai hatua hiyo ilitokana na wakuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kukataa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

John Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais wa Marekani amesema: "Maadamu Wapalestina hawaketi kwenye meza ya mazungumzo na Israel, ofisi ya  PLO mjini Washington haitafunguliwa.

Hatua hii imechukuliwa wiki chache tu baada ya Marekani kukata msaada wa dola milioni 300 kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA).

Riyadh al Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika radiamali yake kufuatia kufungwa ofisi ya PLO nchini Marekani amesema: "Maudhui hii kwa mara nyingine imethibitisha kuwa, Marekani ni mwakilishi wa kipekee na mlinda maslahi ya Israel kote duniani.

Katika hatua nyingine, Marekani imetangaza kukata misaada  ambayo ilikuwa ikitumiwa na Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika mradi wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni. Marekani imesema misaada hiyo sasa itakuwa ikitumwa Israel.  Hatua hizo za Marekani zimekuwa zikichukuliwa kwa lengo la kuwashinikiza Wapalestina ili wakubali kufikia maelewano na utawala ghasibu wa Israel katika fremu ya kile kinachotajwa kuwa ni 'Muamala wa Karne' ambao umependekezwa na Trump.

Haya yanajiri wakati ambao kila siku utawala katili wa Israel unawaua Wapalestina sambamba na kwapokonya haki zao zote ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi katika ardhi zao za jadi. Wapalestina wanashinikizwa ili waachane na mapambano yao ya kupigania ukombozi wa ardhi zao ambazo zinakaliwa kwa mabavu na Israel. Katika hatua nyingine ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeanza kuwatimua Wapalestina katika kijiji cha Khan Al Ahmar katika Ukingo wa Magharibi hatua ambayo imelaaniwa vikali kimataifa. Katika upande mwingine Trump anaendeleza uungaji mkono wake usio na kifani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Rais Trump wa Marekani

Katika kutekeleza matakwa ya utawala wa Israel, Trump ameutambua mji wa Quds au Jerusalem kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na tayari ameshahamisha ubalozi wa nchi yake kutoka Tel Aviv hadi mji huo wenye kibla cha kwanza cha Waislamu hatua ambayo imelaaniwa hata na waitifakie wake barani Ulaya.

Aidha Marekani imeunga mkono mauaji yanayotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya waandamanaji Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza ambao wanashiriki katika maandamano ya amani ya 'Haki ya Kurejea' kila Ijumaa. Trump ameunga mkono mauaji hayo na kusema eti ni haki ya Israel kujilinda. Hii ni katika hali ambayo mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yanasema hatua ya Israel kuwaua Wapalestina wanaoandamana kwa amani ni jinai ya kivita.

Pamoja na kuwa Marekani inauunga mkono kikamilifu utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini utawala huo sasa umezidi kuchukiwa na kutengwa kimataifa.

Tags

Maoni