Sep 18, 2018 14:41 UTC
  • Marekani yakataa kumpatia viza Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina

Gazeti la Al-Akhbar linalochapishwa nchini Lebanon limeripoti kuwa ofisi ya masuala ya viza ya ubalozi wa Marekani mjini Tel Aviv imelikataa ombi la Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina la kupatiwa viza yeye na ujumbe anaoandamana nao kwa ajili ya safari ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Toleo la leo la gazeti hilo limeandika kuwa Mahmoud Abbas na ujumbe anaofuatana nao walipeleka pasi zao za kusafiria ofisi ya masuala ya viza ya ubalozi wa Marekani mjini Tel Aviv kwa ajili ya kwenda kushiriki kikao cha kila mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, lakini ofisi hiyo imetangaza kwamba: Baada ya mabadiliko yaliyojiri hivi karibuni haihusiki na ushughulikiaji wa suala hilo.

Kwa mujibu wa ofisi hiyo, ubalozi wa Marekani mjini Quds ndio unaohusika na utoaji viza na kwamba balozi wa Marekani Israel, David Friedman ndiye anayehusika na suala hilo.

Husam Zomlot, balozi wa Palestina nchini Marekani

Hata hivyo kutokana na msimamo wa Mahmoud Abbas kugongana na ule wa balozi huyo wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekataa kuwasiliana naye kwa ajili ya suala hilo.

Kabla ya hapo serikali ya Marekani ilichukua hatua ya kuifunga ofisi ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) mjini Washington na kubatilisha kibali ya kuishi nchini humo cha balozi wa Palestina Dr. Husam Zomlot pamoja na familia yake. Licha ya kibali hicho kuwa na muda hadi mwaka 2020, lakini balozi huyo wa Palestina ametakiwa yeye na familia yake waondoke haraka katika ardhi ya Marekani.../

Maoni