Sep 19, 2018 06:23 UTC
  • Mashambulizi ya anga ya Saudia yaua wavuvi 18 wa Yemen

Wavuvi wasiopungua 18 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya ndege za kivita za Saudi Arabia dhidi ya boti za wavuvi hao katika mji wa Pwani wa Khokha, magharibi mwa mkoa wa Hudaydah.

Harakati ya Ansarullah ya Yemen imeripoti katika tovuti yake kwamba, ndege hizo za kivita za Saudia zilifanya hujuma hiyo jana Jumanne nyakati za jioni, katika mji wa Khokha yapata kilomita 90 kusini mwa mkoa wa Hudaydah. Habari zaidi zinasema kuwa, mvuvi mmoja tu ndiye aliyenusurika katika mashambulizi hayo ya kikatili ya ndege za kijeshi za Saudi Arabia.

Mbali na mauaji hayo ya Khokha, raia wawili waliuawa katika hujuma nyingine ya anga ya Riyadh dhidi ya maeneo ya makazi ya watu katika wilaya ya Durayhimi mkoani Hudaydah.

Kadhalika hapo jana vifaru vya Saudi vilivurumisha maroketi dhidi ya wakazi wa wilaya ya Razih, katika mkoa wenye milima mingi wa Sa'ada, ulioko kaskazini magharibi mwa nchi. Idadi ya wahanga wa shambulizi hilo haijabainika kufikia sasa.

Bandari ya Hudaydah

Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani, Israel, Imarati na nchi nyingine kadhaa iliivamia  kijeshi Yemen mwezi Machi mwaka 2015, na hadi sasa maelfu ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.

Mbali na mauaji, mzingiro mkubwa wa Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen umeifanya nchi hiyo maskini ya Kiarabu ikabiliwe na uhaba mkubwa wa chakula, dawa na kukumbwa na milipuko ya magonjwa ya aina mbalimbali na hivyo kusababisha maafa ya kibinadamu. 

Tags

Maoni