Sep 19, 2018 14:44 UTC
  • Ismail Hania: Maandamano ya Haki ya Kurejea na kuondolewa mzingiro hayatasimama

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, taifa la Palestina limeazimia kwamba, litasimama kidete kukabiliana na mzingiro wa adui Mzayuni hadi pale litakapousambaratisha.

Ismail Hania amesema hayo leo katika shughuli ya kuusindikiza mwili wa shahid Ahmar Omar huko Gaza na kubainisha kwamba, maandamano makubwa ya haki ya kurejea katika mipaka ya Ukanda wa Gaza hayatasimama hadi pale mzingiro dhidi ya eneo hilo utakapoondolewa na kufikia tamati taabu na masaibu ya wakazi hao.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameeleza kuwa, wakazi wa Gaza wameazimia kuhitimisha njama za maadui dhidi yao.

Maandamano ya Wapalestina ya "Haki ya Kurejea"

Ameongeza kuwa, taifa shujaa la Palestina limeingia katika vita viwili ambapo vita vya kwanza ni kuushinda na kuusambaratisha mzingiro na vita vya pili ni kupigania haki ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi zao za asili pamoja na kukabiliana na suala la kukatwa misaada ya Marekani kwa ajili ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Maandamano ya amani yaliyopewa jina la "Haki ya Kurejea" yalianza tarehe 30 Machi mwaka huu kwa mnasaba wa Siku ya Ardhi huko Ukanda wa Gaza na yangali yanaendelea.

Tangu wakati huo hadi sasa zaidi ya Wapalestina 150 wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na wengine 17,500 wamejeruhiwa.

Tags

Maoni