Sep 21, 2018 02:48 UTC
  • Sababu na malengo ya vikao vya siri dhidi ya Palestina huko Imarati

Mtandao wa habari wa Khaleej Online umefichua kwamba, Imarati ni mwenyeji wa vikao vya siri dhidi ya Palestina vinavyofanyika kwa shabaha ya kubadili malengo ya mapambano ya Wapalestina.

Inaonekana kuwa, sababu kuu ya vikao hivyo vinavyofanyika huko Abu Dhabi ni kushindwa serikali ya Donald Trump kufikia malengo yake na kutekeleza kile kilichopewa jina la "Muamala wa Karne". Serikali ya Trump ilikusudia kuziyahudisha kikamilifu ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kupitia utekelezaji wa mpango huo habithi. Hata hivyo mpango huo umekataliwa na makundi yote ya Palestina. Si hatu tu bali hata Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekata uhusiano wake na Marekani na imekataa kurejea kwenye meza ya mazungumzo na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kuhusu swali kwamba, ni nani wahusika wakuu katika vikao hivyo vya Abu Dhabi?, ni kwamba maafisa wa Saudi Arabia, Imarati, Misri, baadhi ya wanasiasa wa Kipalestina wanaoishi nje na maafisa wa serikali ya Donald Trump ndio wanaoshiriki vikao hivyo. Hadi sasa kumefanyika vikao vitatu vya siri huko Abu Dhabi na Khaleej Online inaripoti kuwa, maafisa wa serikali ya Palestina na PLO hawashirikishwi katika vikao hivyo. Suala hili la kutoshirikishwa maafisa wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina au harakati ya PLO inadhihirisha wazi hakika ya vikao hivyo.  

Vikao vya siri dhidi ya palestina vinafanyika Imarati

Kuhusu malengo yake, inaonekana kuwa ni kubuni chombo mbadala cha serikali ya sasa ya Palestina ili iwapo Mamlaka ya Ndani ya Palestina itaendelea kupinga mpango wa Trump wa "Muamala wa Karne", iwekwe chini ya mashinikizo makali na hatimaye kuwekwa kando. Ni kwa sababu hii ndiyo maana wanasiasa wa Kipalestina wanaoishi nje ya nchi wanashiriki kwa wingi katika  vikao hivyo vya siri.

Inaonekana pia kwamba, lengo jingine la vikao hivyo ni kuokoa mpango wa Muamala wa Karne wenyewe. Japokuwa baadhi ya vipengee muhimu vya mpango huo wa Muamala wa Karne kama vile kadhia ya kuutambua mji wa Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel na kuhamishiwa ubalozi wa Marekani katika mji huo kutoka Tel Aviv, vimetekelezwa, lakini kutokana na kwamba mpango huo kwa ujumla unapingwa na makundi makubwa ya Wapalestina haujaweza kufikia malengo yake. Ni kwa kutilia maanani ukweli huo ndiyo maana mtandao wa Khaleej Online ukaripoti kuwa: "Katika vikao vya siri vya Abu Dhabi kutachukuliwa maamuzi juu ya jinsi ya kuwawekea mashinikizo zaido Wapalestina kwa ajili ya kubadili misimamo yao ya kisiasa kuhusu utawala haramu wa Israel na Marekani na kubadili mtazamo wao juu ya suala la kuwa na uhusiano wao na Israel."

Image Caption

Sera zilizodhidi ya Palestina za watawala wa Imarati si jambo jipya na geni. Kwa ujumla watawala wa Imarati ambao ni vibaraka na wanasesere wa Marekani hawana siasa huru kuhusu masuala muhimu ya Mashariki ya Kati hususan kadhia ya Palestina. Imarati ni miongoni mwa nchi chache sana zilizokubali mpango wa Trump wa Muamala wa Karne na ina uhusiano rasmi wa siri na wa wazi na utawala wa Kizayuni wa Israel. Baadhi ya duru pia zimefuchua kuwa, Imarati na Israel zimeshirikiana katika operesheni za kigaidi zinazowalenga wapigania uhuru wa Kipalestina. Katika mkondo huo Jumuiya ya Kiarabu ya Kutetea Haki za Binadamu yenye makao yake nchini Uingereza mwezi Juni mwaka uliopita wa 2017 ilifichua kwamba, kwa uchache watu wawili wa timu iliyoshiriki katika mauaji ya Mahmoud Mabhuh ambaye alikuwa kiongozi wa ngazi ya juu katika Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS), wanaishi kwa uhuru kamili nchini Imarati. Mabhuh aliuawa tarehe 19 Januari mwaka 2010 katika shambulizi la kigaidi akiwa katika hoteli moja huko Dubai.    

Maoni