Sep 21, 2018 07:53 UTC
  • Mazungumzo ya Waziri Mkuu wa Pakistan na viongozi wa Saudi Arabia

Katika safari yake nchini Saudi Arabia Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan amekutana na kufanya mazungumzo na Mfalme Salman bin Abdul Aziz pamoja na Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo.

Vyombo vya habari vya Saudi Arabia sambamba na kuakisi habari ya mazungumzo ya Imran Khan na viongozi wa Riyadh, vimetosheka tu na kutaja maudhui jumla kuhusiana na mazungumzo ya pande mbili likiwemo suala la hamu ya kila upande ya kuimarisha uhusiano na upande wa pili sanjari na kujadliana masuala ya pamoja, ya kieneo na kimataifa.

Kabla ya mazungumzo yake na Mfalme na mrithi wa kiti cha ufalme, Waziri Mkuu mpya wa Pakistan alikutana na kufanya mazungumzo na Khalid bin Abdul Aziz al-Falih, Waziri wa Nishati, Viwanda na Madini, Yasir Al-Rumayyan, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Umma wa Uwekezaji Vitega Uchumi wa Saudi Arabia pamoja na Yusuf Bin Ahmed Al-Uthaymeen, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan katika mazungumzo yake na Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia

Waziri Mkuu wa Pakistan ameichagua Saudi Arabia kuwa kituo chake cha kwanza cha safari ya nje ya nchi baada ya kushika wadhifa huo, katika hali ambayo, kabla ya safari hiyo, Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia alimpigia simu Imran Khan mara tatu katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja.

Kwa hakika baada ya Chama cha Tehreek-e-Insaf kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge nchini Pakistan mwezi Julai, suala la muelekeo mpya katika sera za kigeni za nchi hiyo hususan uhusiano wa Islamabad na Riyadh ni jambo ambalo lilitawala katika duru za kisiasa na kihabari za kieneo. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, uhusiano wa Saudi Arabia na Pakistan tangu kale na hasa katika kipindi cha utawala wa Chama cha Muslim League cha Nawaz Sharif ulichukua mkondo wa kuboreka zaidi.

Kushika hatamu za uongozi Chama cha Tehreek-e-Insaf nchini Pakistan na kushuhudiwa kupigwa kumbo Chama cha Muslim League kuliutia wasiwasi utawala wa Riyadh na kuwa na unyeti maalumu kuhusiana na mustakabali wa uhusiano wake na Islamabad. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana, Muhammad bin Salman amezungumza kwa njia ya simu na Imran Khan mara tatu katika kipindi cha mwezi mmoja.

Khalid al-Falih, Waziri wa Nishati, Viwanda na Madini wa Saudi Arabia akimkaribisha Imran Khan Waziri Mkuu wa Pakistan

Saudi Arabia ikiwa na lengo la kuimarisha sehemu ya uwezo wa operesheni za makundi ya kigaidi katika nchi mbalimbali za eneo inategemea sana suala la kuwapatia mafunzo vijana katika shule za Kiislamu nchini Pakistan ambazo zinaeneza fikra za kufurutu ada. Ndio maana imewekeza na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kupanua na kueneza shule hizo nchini Pakistan.

Baada ya kuingia madarakani huko Pakistan Chama cha Tehreek-e-Insaf cha Imran Khan, nyota wa zamani wa mchezo wa kriketi, viongozi wa Riyadh wanahaha na kufanya kila wawezalo ili kupitia njia ya mazungumzo na serikali mpya ya Islamabad na kwa kisingizio cha misaada ya kifedha kwa vituo vya kiutamaduni na kielimu nchini humo, waweze kuzitumia shule hizo kama vituo vya kulea watu wenye fikra za Uwahabi.

Kadhalika viongozi wa Saudi Arabia wanataka kutumia njia ya mazungumzo na kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi na serikali ya Pakistan ili waifanye misimamo ya viongozi wa Islamabad iendane na siasa zao za chokochoko na uharibifu katika Mashariki ya Kati. 

Saudi Arabia imeanzisha na inadhamini madrasa za Kiwahabi nchini Pakistan

Hapana shaka kuwa, kuwaridhisha viongozi wa Pakistan na kuwafanya washirikiane na Saudi Arabia katika vita dhidi ya wananchi madhulumu wa Yemen ni miongoni mwa malengo yanayofuatiliwa na viongozi wa Riyadh kwa sasa.

Licha ya kuweko mlolongo wa matarajio ya viongozi wa Riyadh ya kushirikiana na serikali mpya ya Pakistan, lakini wananchi wa nchi hiyo wanataraji kumuona Imran Khan na serikali yake wakitekeleza ahadi za wakati wa kampeni za uchaguzi ikiwemo ya kudhamini maslahi ya taifa na kuimarisha uhusiano na nchi jirani na hivyo kutonasa katika mtego wa siasa za  Saudi Arabia za kuzusha mivutano katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kwa kuzingatia misimamo ya Imran Khan na umakini wake katika kufuata siasa za kimantiki katika sera za kigeni, ni jambo lililo mbali kumuona Waziri Mkuu huyo mpya akitumbukia katika mtego ulioandaliwa na Saudi Arabia.

Tags

Maoni