• Fikra ya Ashura ya watu wa Yemen, ngome imara dhidi ya maadui

Jana Alkhamisi maelfu ya watu wa Yemen walijitokeza kwa wingi kushiriki matembezi ya Siku ya Ashura katika miji ya Sanaa na Sa'da na kwa mara nyingine tena kusisitiza juu ya udharura wa kusimama imara mbele ya wavamizi na wachokozi.

Washiriki wa matembezi hayo walisisitiza kwamba Imam Hussein (as) ni nembo muhimu ya mapambano katika historia ya Uislamu na jamii nzima ya mwanadamu na kwamba Wayemen wanapata ilhamu na nguvu zao za mapambano dhidi ya adui kutokana na nembo hiyo muhimu na tukufu ya Ashura. Matukio ya kihistoria yanabainisha wazi kwamba licha ya kupita zaidi ya miaka 1400, lakini bado bendera ya mapambano dhidi ya dhulma na mapenzi kwa Imam Hussein (as) ingali inapepea kwa izza na utukufu miongoni mwa vizazi tofauti vya jamii ya mwanadamu. Kwa kutegemea utamaduni tajiri wa Ashura, wanapambano shupavu wa Yemen licha ya kutokuwa na zana za kivita za kutosha, wameweza kudumisha mapambano yao dhidi ya wavamizi wa nchi yao waliojizatiti vilivyo kwa silaha za kisasa na hivyo kuwashangaza walimwengu kwa ujasiri wao mkubwa mbele ya adui. Mafundisho ya Ushia ya kupigania uhuru yamesimama juu ya msingi wa kupigana na kila aina ya dhulma na ubeberu na hilo ndilo jambo linalowapa nguvu na azma watu wa Yemen ya kuendelea kusimama imara na kupambana kishujaa na ubeberu pamoja na udikteta.

Mamilioni ya Wayemen wakiandamana kupinga uvamizi wa Saudia dhidi ya nchi yao

Marekani na utawala wa Saudia Arabia zinachukulia fikra na mafundisho haya kuwa kizuizi kukibwa katika njia ya kutekeleza siasa zao za kibeberu katika eneo na ndio maana zikaamua kutumia kila mbinu na njama kuzima fikra hii ya Uislamu halisi na hasa wa Kishia na wa wafuasi wa Ahlul Beit  wa Mtume (as) ili kujaribu kuzima moto wa mapambano dhidi ya maadui hao wa Uislamu na kuandaa njia ya kufikiwa malengo yao haramu katika eneo. Pamoja na hayo lakini uzoefu unaoonyesha kwamba utamaduni unaoimarika kila siku wa Ashura kamwe hauwezi kuzimwa. Kwa kuanzisha hamasa na mapambano ya Ashura, Imam Hussein (as) katika kipindi chote cha historia ametokea kuwa mfano bora unapoaswa kuigwa na kila mpenda amani, auadilifu na uhuru duniani. Kuhusiana na suala hilo, Hujjatul Islam wal Muslimeen, mtaalamu wa masuala ya kiutamaduni anasema kwamba baada ya tukio chungu na la kuhuzunisha la Ashura katika jangwa la Karbalaa nchini Iraq, kila Mwislamu aliye na fikra huru na mpigania amani  wa kweli, anakichukulia kimya mbele ya taghuti na dhalimu kuwa jambo la aibu na kushirikiana naye kuwa dhambi kubwa. Anaendelea kusema kuwa Ashura imepelekea kuimarishwa moyo wa kupigania haki mbele ya madhalimu ambapo harakati ya Ashura  inakichukulia kifo cha utukufu kuwa mwanzo wa maisha ya heshima na izza. Utamaduni huu wa Ashura ambao sasa umeenea katika pembe tofauti za dunia, unatufundisha kwamba  ili kupambana na mataghuti na madhalimu tunapasa kutumia kila njia na suhula.

Ashura

Matukio ya Yemen yanabainisha wazi kwamba watawala wa Aal Saud na waungaji mkono wao wa Magharibi wameshindwa kabisa kisiasa, kijeshi na kimaadili katika vita vyao vya kichokozi dhidi ya taifa la Yemen. Saudia ambayo ilianzisha vita hivyo dhidi ya Yemen tarehe 26 mwezi Machi 2015 ikidhani kuwa ingeweza kuisambaratisha nchi hiyo masikini katika kipindi kifupi na hivyo kufikia lengo lake la kumrejesha madarakani rais mtoro wa nchi hiyo Abdurabbu Mansurhadi, imetambua kwamba ilifanya makosa makubwa kuhusiana na vita hivyo ambavyo sasa vimeingia katika mwaka wake wa nne. Kosa la msingi lililofanywa na Saudia na washirika wake wa Magharibi ni kwamba walipuuza nguvu kubwa ya mapambano ya watu wa Yemen wakiongozwa na wapiganaji wa Ansarullah ambao wanaendesha mapambano yao hayo kwa msingi wa mafudisho ya Ashura. Wapiganaji hao wameweza kuwasababisha maafa na hasara kubwa wavamizi wa Saudia na vibaraka wao ndani na nje ya mipaka ya Yemen.

Sehemu ya uharibifu unaofanywa na hujuma ya Saudia nchini Yemen

Licha ya kuwa na zana za kisasa kabisa za vita na uwezo mkubwa wa kifedha pamoja na uungaji mkono wa kibeberu wa nchi za Magharibi, lakini Wasaudia wameshindwa kabisa kufikia malengo yao nchini Yemen na hili linatokana na ukweli kwamba nguvu ya kijeshi haiwezi kuishinda nguvu ya imani. Sifa hii muhimu ya imani walionayo watu wa Yemen imekuwa ngome thabiti na imara mbele ya maadui, ambayo imewapelekea kukwama kabisa katika kinamasi cha nchi hiyo masikini.

Tags

Sep 21, 2018 13:17 UTC
Maoni