Sep 22, 2018 16:46 UTC
  • El Baradei akosoa vitisho vya Trump dhidi ya nchi za Kiarabu

Mwanasiasa mashuhuri wa Misri amemkosoa rais wa Marekani kwa kutoa vitisho dhidi ya nchi za Kiarabu.

Muhammad el Baradei, mwanasiasa mashuhuri wa Misiri na Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ameandika katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kwamba: Kwa masikitiko, rais wa Marekani Donald Trump anaendelea kutoa vitisho kwa nchi za Kiarabu. Kisingizio chake ni kwamba Marekani inawahami Waarabu na kwamba Waarabu nao wanapaswa kutii amri zake.

El Baradei ameongeza kuwa, matusi yanayoendelea kutolewa na Trump huenda katika siku za usoni yakazifanya baadhi ya nchi za Kiarabu na zisizo za Kiarabu zilazimike kujitafutia ngao maalumu ya kujihami; na hatua hiyo itakuwa na taathira kadhaa kwa usalama wa dunia.

Rais Donald Trump wa Marekani

Hivi karibuni, Trump alizitaka nchi za Kiarabu zishushe bei ya mafuta.

Kwa kutumia lugha ya vitisho, rais huyo wa Marekani amesema, nchi yake inazihami nchi za Mashariki ya Kati na kwamba bila ya Marekani nchi hizo haziwezi kuwa katika amani na usalama hata kwa muda mfupi.

Trump ameongeza kuwa jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta duniani OPEC ambayo ndiyo inayodhibiti masoko ya mafuta inapaswa kushuha haraka bei ya bidhaa hiyo.../

Maoni