Sep 23, 2018 07:52 UTC
  • Imarati yaondoa kikosi cha mwisho cha askari wake Yemen

Kikosi cha mwisho cha wanajeshi wa Umoja wa Falme za Kiarabu kilichokuwa kikihudumu chini ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika mkoa wa Mahran nchini Yemen kimewasili nyumbani baada ya serikali ya Abu Dhabi kukiagizi kiondoke katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Duru za kuaminika zimeiambia kanali ya televisheni ya Yemen ya Shabab kwamba, Imarati imewaondoa wanajeshi hao mkoani Mahran na kuwakabidhi viongozi wa eneo hilo nyumba zilizokuwa zikitumiwa na askari hao wa UAE.

Habari zaidi zinasema kuwa, Abu Dhabi inatazamiwa kuwatuma mamluki na washauri wa kijeshi kutoka nchi za Afrika kwenda kuchukua nafasi ya kikosi chake hicho.

Muungano huo vamizi umekuwa ukiwatumia mamluki kutoka nchi za Afrika kama vile Sudan katika mashambulizi yake dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Yemen.

Askari wa Sudan nchini Yemen

Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwaka jana, harakati ya Ansarullah ya Yemen ilitishia kuishambulia jamhuri iliyojitangazia uhuru ya Somaliland kutokana na hatua yake ya kushirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu dhidi ya wapiganaji wa harakati hiyo ya wananchi.

Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani, Israel, Imarati na nchi nyingine kadhaa iliivamia Yemen mwezi Machi mwaka 2015 na hadi  sasa raia zaidi ya 15,000 wasio na hatia, hasa watoto na wanawake wa  nchi hiyo wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Tags

Maoni