Sep 23, 2018 12:23 UTC
  • Makubaliano ya mamufti wa Asia ya Kati juu ya kufunguliwa tena shule za kidini

Mamufti wakuu wa nchi nne za Kyrgyzstan, Kazakhstan, Tajikistan na Uzbekistan wamekutana Bishkek, mji mkuu wa Kyrgyzstan na kusaini makubaliano ya kufunguliwa tena shule za kidini katika eneo la Asia ya Kati.


Sambamba na kikao hicho cha Bishkek, wawakilishi wa nchi hizo pia wamekutana mjini Ashgabat, mji mkuu wa Turkmenistan katika kikao cha kujadili njia za kupambana na makundi yenye kufurutu ada na ya kigaidi. Washiriki katika vikao viwili vya Bishkek na Ashgabat wameeleza wasiwasi wao kuhusu ya ongezeko la makundi yenye kufurutu ada na ya kigaidi yanayoingia katika nchi hizo kutoka nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi,  Hii sio mara ya kwanza ambapo viongozi wa serikali za nchi za Asia ya Kati wananakutana na kueleza wasiwasi wao kuhusiana na ongezeko la makundi ya kigaidi.

Kikao cha mamufti wa nchi nne za Asia ya Kati Bishkek 

Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita hususan baada ya kushindwa makundi ya ukufurishaji na ya kigaidi huko Iraq na Syria, Marekani na washirika wake wa Kiarabu wamefanya juhudi kubwa kuifanya Afghanistan ambayo imegubikwa na hali ya mchafukoge kuwa ngome kuu ya makundi hayo ya kigaidi. Kupakana kwa nchi za Asia ya Kati na Afghanistan, kukusanyika kwa idadi kubwa ya wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh huko kaskazini mwa Afghanistan na kadhalika uchache wa maarifa ya dini ya Kiislamu wa mataifa ya Asia ya Kati ni mambo ambayo yamewazidishia wasiwasi mkubwa viongozi wa eneo hilo. Ni kwa msingi huo ndio maana juhudi za pamoja na pia ushirikiano kati ya viongozi hao vikatajwa kuwa njia pekee ya kuweza kukabiliana na tishio la kigaidi katika eneo la Asia ya Kati.

Vilevile harakati za makundi ya kigaidi na yenye kufurutu ada zinazoungwa mkono nchi za Kiarabu hususan utawala wa kifalme wa Aal-Saud nchini Saudi Arabia, Imarati, Kuwait na Jordan, zimezilazimisha baadhi ya nchi za Asia ya Kati kuchukua uamuzi wa kukabiliana na fikra hizo zinazoeneza sumu katika jamii.

Saudia, muenezaji mkuu wa fikra za Uwahabi katika nchi za Asia ya Kati

Katika uwanja huo, viongozi wanaohusika na elimu na vyuo vikuu katika nchi za Asia ya Kati wameingia rasmi katika mapambano dhidi ya fikra hizo zenye sumu na zisizofaa. Katika uwanja huo suala la kufunguliwa tena shule za kidini ni jambo ambalo lilikuwa likisisitizwa sana na viongozi wa Asia ya Kati licha ya kwamba baadhi ya serikali za eneo hilo zimekuwa wasiwasi kuhusu njia na namna ya kukabiliana na makundi ya kigaidi na yenye misimamo mikali. Vladimir Ashkolny, mkuu wa Kitengo cha Utamaduni wa Dunia katika chuo cha Kyrgyzstan anaamini kwamba, propaganda za makundi ya kufurutu ada, ni hatari kubwa kwa usalama wa nchi za Jamhuri za Asia ya Kati na lengo kuu la makundi hayo potofu ni kuwapotosha wanafunzi, wasomi wa vyuo vikuu na nguvukazi ya vijana. Kwa mujibu wa Ashkolny, kutoandaliwa mazingira bora na mahitajio ya kirohoi na kidini kwa vijana na pia kutojibiwa maswali yao, kumepelekea kujitokeza pengo la kifikra miongoni mwa vijana wa nchi za Asia ya Kati na katika hali hiyo hatari ya kukaririshwa fikra potofu inatishia mustakbali wa vijana wa eneo hilo.

Ukweli ni kwamba, katika hali hiyo inaonekana kwamba walinganiaji wa kundi la Kiwahabi wanatumia mwanya huo katika kueneza fikra za kundi hilo katika eneo tajwa.

Maoni