• Maandamano ya

Yahya Sinwar, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS katika Ukanda wa Gaza amesisitiza kuwa Ukanda wa Gaza ni njia ya mapambano yanayoendelea.

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas katika Ukanda wa Gaza amebainisha kuwa maandamano makubwa ya Haki ya Kurejea katika eneo la mpaka wa Gaza ni njia ya mapambano yanayoendelea, yanayopanuka zaidi siku baada ya siku hadi yatakapofikiwa malengo aali ya taifa la Palestina ambayo ni kuikomboa Palestina na uvamizi na ukaliwaji wa mabavu, kurejea wakimbizi wa Kipalestina na kuuvunja mzingiro wa Gaza. Muqawama wa kiraia wa wananchi wa Palestina unaoendeshwa kwa sura ya maandamano ya kurejea Wapalestina, unaendelea katika hali ambayo wananchi hao madhulumu wasio na ulinzi wanakabiliwa na hatua kali kabisa za ukandamizaji na ukatili za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Yahya Sinwar, Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, Gaza

Hatua za utawala wa Kizayuni zimedhihirisha upeo wa ushenzi na unyama wa utawala huo ghasibu ambao umepatwa na hofu na kiwewe cha kupamba moto Intifadha ya wananchi wa Palestina inayoendelezwa kwa sura tofauti. Wakati Marekani, Israel na baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu walikuwa wanafanya juu chini kuubadilisha mlingano wa kimataifa  kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni wa Israel kupitia mpango wa Muamala wa Karne, Wapalestina wametumia uwezo na nyenzo za muqawama ikiwemo ya Maandamano ya Haki ya Kurejea kuanzisha vuguvugu jengine jipya la kukabiliana na njama dhidi ya Palestina. Moja ya matunda ya Maandamano ya Kurejea ni kutoa mguso na kupewa umuhimu kadhia ya Palestina ambayo ilikuwa imewekwa kando kutokana na matukio mengine ya eneo. Mafanikio mengine ya vuguvugu hilo ni ulimwengu kulipa umuhimu zaidi suala la udharura wa kuondolewa mzingiro wa Gaza ulioanzishwa na utawala dhalimu wa Israel mwaka 2007 na kuendelezwa hadi sasa. Kwa hivyo harakati mpya iliyoanzishwa na Wapalestina imezidi kuanika hatua za kidhalimu za Wazayuni maghasibu na kuonyesha umuhimu wa kuondolewa mzingiro wa kionevu dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza.

Licha ya jinai na umwagaji damu unaofanywa na utawala dhalimu wa Kizayuni vijana Wapalestina wanaendeleza Muqawama wa Maandamano Makubwa ya Haki ya Kurejea

Ukweli ni kwamba vuguvugu kubwa la Wapalestina linaloendeshwa kwa sura ya Maandamano ya Kurejea ni sisitizo la kuendelezwa muqawama na kusimama kwao imara kukabiliana na Wazayuni maghasibu kwa mbinu na njia tofauti. Kwa upande wa ndani, Maandamano ya Haki ya Kurejea yamezidi kuukanganya utawala wa Kizayuni na kuufanya ushindwe kukabiliana na muqawama wa wananchi wa Palestina. Kushindwa huko kumeongezeka maradufu hasa kutokana na hatua nyingine za kimuqawama zilizochukuliwa na Wapalestina kujibu jinai za kila uchao zinazofanywa na Israel. Maandamano ya Haki ya Kurejea sambamba na majibu ya mashambulio ya makombora ya Muqawama wa Palestina kwa jinai na uchokozi wa Israel vimezidi kuwavunja nguvu Wazayuni hao maghasibu katika kukabiliana na nyenzo tofauti za muqawama wa wananchi wa Palestina, kuanzia muqawama wa harakati za kiraia hadi ule wa mapambano ya mtutu wa bunduki.

Taswira ya mshikamano wa Wapalestina katika Maandamano Makubwa ya Kurejea

Duru nyingi za habari na mitandao ikiwemo tovuti ya habari na uchambuzi ya Middle East Eye zimeyaelezea Maandamano ya Haki ya Kurejea kama tajiriba mpya na endelevu katika njia ya Muqawama wa Wapalestina. "Maandamano Makubwa ya Kurejea" ya Gaza ni hatua muhimu mno katika mbinu za mapambano ya Wapalestina. Vuguvugu hilo limevutia mshikamano wa kimataifa wa kutetea na kuunga mkono haki za Wapalestina na kupewa umuhimu zaidi kadhia ya Palestina na jamii ya kimataifa. 

Nukta ya kuzingatiwa ni kwamba kushadidi ukatili unaofanywa na Israel dhidi ya maandamano makubwa ya haki ya kurejea, si tu hakujaweza kuzima harakati hiyo ya upinzani lakini kumesababisha pia kupamba moto muqawama katika maeneo mengine ya Palestina likiwemo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan. Mabadiliko yote hayo yanadhihirisha nguvu ya kitaifa ya Wapalestina katika kukabiliana na madhila ya kufanywa wakimbizi sambamba na kuvamiwa ardhi zao na kukaliwa kwa mabavu. Lakini pia yametoa mwanga wa matumaini wa kufikiwa malengo matukufu ya Palestina chini ya mhimili wa muqawama endelevu wa kukabiliana Wazayuni maghasibu sambamba na kuufanya mlingano wa nguvu katika uga wa kimataifa ubadilike kwa manufaa ya Palestina.../

Sep 24, 2018 07:24 UTC
Maoni