Sep 25, 2018 13:58 UTC
  • Mchango muhimu wa Hizbullah katika ushindi wa Lebanon dhidi ya ugaidi

Rais Michel Aoun wa Lebanon ametetea uwepo wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon huko nchini Syria na kusema kuwa, uwepo huo ni kwa ajili ya kuihami nchi yake na hujuma za magaidi.

Rais Michel Aoun alisema hayo Jumatatu ya jana katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Ufaransa la Le Figaro na kubainisha kwamba, baadhi ya watu wanalaani uingiliaji wa Hizbullah katika vita na makundi ya kigaidi ya Daesh na Jabhat al-Nusra nchini Syria, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, magaidi wamevamia ardhi yetu na Hizbullah ndiyo iliyoihami na kuitetea Lebanon.

Hizbullah ya Lebanon ni moja ya viungo vikuu na asili vya nguvu ya Lebanon katika kukabiliana na njama mbalimbali na ni moja ya vigezo vikuu vinavyounda pembe tatu ya dhahabu ya kiulinzi ya nchi hiyo yaani jeshi, wananchi na muqawama. Kwa hakika mihimili hiyo mikuu mitatu ndio siri ya mafanikio ya Lebanon na kuvuka nchi hiyo kila kizingiti na mazinga hatari.

Juhudi za kiulinzi za Lebanon hususan muqawama wa Kiislamu zilizaa matunda tarehe 26 Agosti mwaka jana baada ya nchi hiyo kufanikiwa kuisafisha ardhi yake kikamilifu na uwepo wa makundi ya kigaidi.

Wanamuqawama wa Hizbullah ya Lebanom

Hapana shaka kuwa, kusafishwa kikamilifu na uwepo wa magaidi maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na magaidi katika mipaka ya Syria na Lebanon kuliharakisha mwenendo wa kuishindwa magaidi hao katika nchi mbili hizo. Mafanikio ya Lebanon dhidi ya magaidi chini ya anuani ya "Ukombozi wa Pili" yalipatikana katika hali ambayo, vikosi vya muqawama vikishirikiana na jeshi la Lebanon vilikuwa vimeweza kuyakomboa maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo yaliyokuwa katika mikono na udhibiti wa makundi ya kigaidi na kitakfiri.

Tukio hilo linatajwa nchini Lebanon kama "Ukombozi wa Pili" baada ya kukombolewa maeneo muhimu ya nchi hiyo kutoka katika udhibiti wa utawala vamizi wa Israel mwaka 2000. Nchi ya Lebanon ikiwa jirani wa Syria imedhurika na kuathirika pakubwa na vita vya kutwishwa jirani yake yaani Syria. Baada ya magaidi kushindwa kufikia malengo yao nchini Syria walianza kuilenga Lebanon kwa wimbi la mashambulio ya kigaidi ili kuleta vurugu na machafuko katika nchi hiyo na wakati huo huo, kudhamini maslahi ya waungaji mkono wao wa Kiarabu na Kimagharibi.

Pamoja na hayo, kutokana na uungaji mkono kamili wa serikali, wananchi na muqawama wa Lebanon kwa jeshi la nchi hiyo, makundi ya kigaidi na kitakfiri baada ya kuchezea vipigo mtawalia nchini Lebanon katika miaka ya hivi karibuni, yamelazimika kuondoka katika maeneo yote ya mpakani mwa nchi hiyo na kuingia katika ardhi ya Syria.

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Jabhat al-Nusra

Hata hivyo kutokana na kuweko uratibu kamili baina ya Hizbullah na jeshi la Lebanon katika vita na magaidi katika maeneo ya mpakani hususan hatua makini na za uweledi za Hizbullah katika kuwasaka na kuwafuatilia magaidi hao ndani ya ardhi ya Syria, makundi hayo ya kigaidi yanayoungwa mkono na baadhi ya madola ya Magharibi na ya eneo la Mashariki ya Kati yameshindwa kabisa kufurukuta nchini Lebanon na kuwa na harakati zenye wigo mpana katika nchi hiyo kinyume na  nchini Syria na Iraq.

Mtandao wa Habari wa al-Ahad umeandika, kuingia Hizbullah ya Lebanon nchini Syria ilikuwa nukta muuhimu na kubwa ya mabadiliko ambayo ilisambaratisha njama zilizokuwa zimepangwa na kuratibiwa kwa ajili ya eneo la Mashariki ya Kati na hivyo kuzitupa njama hizo katika debe la taka. Kwa upande mwingine, uwepo wa vikosi vya Hizbullah ya Lebanon nchini Syria kulileta matumaini kwa wananchi wa nchi nyingine ikiwemo Yemen, Bahrain na Palestina. Kwa hakika Hizbullah imejisajili katika historia kama nembo ya uushindi.

Rais Bashar al-Assad wa Syria

Hatua ya Lebanon ya kutegemea jeshi na muqawama wa wananchi kwa uongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah kumepelekea kusamabaratishwa njama za magaidi na utawala haramu wa Israel dhidi ya nchi hiyo na filihali Lebanon imegeuka na kuwa kikwazo na kizingiti imara mbele ya hatua za kupenda kujitanua na za kuzusha fitina na fakachi za Israel na magaidi wa kitakfiri katika eneo la Mashariki ya Kati.

Katika uwanja huo, Hizbullah imekuwa na nafasi mchango muhimu mno,  mchango ambao daima umekuwa ukitukuzwa na kuthaminiwa na viongozi wa Lebanon; na hata matamshi ya Rais Michel Aoun wa nchi hiyo yanaweza kutathminiwa katika uwanja huo.

Tags

Maoni