Oct 15, 2018 04:46 UTC
  • Serikali ya Qatar nayo yaitaka Saudi Arabia kueleza walipo raia wake waliotekwa nyara na nchi hiyo

Huku dunia ikiwa bado inaishinikiza Saudia kuweka wazi hatma ya mwandishi wa habari na mkosoaji wake aliyetoweka katika ubalozi wa nchi hiyo nchini Uturuki, serikali ya Qatar kupitia mkuu wa kamisheni ya kitaifa ya haki za binaadamu, ameitaka Riyadh kuieleza Doha kuhusu hatma ya raia wake waliotekwa nyara na utawala wa Aal Saud.

Ali Bin Samikh al-Marri, na bila ya kuashiria majina ya raia hao wa Qatar waliotekwa nyara na Saudia amesema kuwa, jukumu la kulindwa usalama wa wahanga waliokamatwa kwa lazima na kutoweka liko mikononi mwa nchi hiyo. Aidha sambamba na kukitaja kitendo hicho cha Saudia kuwa cha kijeuri,  Mkuu wa Kamisheni ya Kitaifa ya Haki za Binaadamu nchini Qatar ameutaka Umoja wa Mataifa kusaidia kubainika hatma ya raia wake waliotekwa nyara na Saudia na kuongeza kuwa, licha ya kuwepo juhudi zinazofanywa na kamisheni hiyo kwa kushirikiana na familia za wahanga, lakini hadi sasa serikali ya Doha haijaweza kupata taarifa zozote za raia wake hao. Ali Bin Samikh al-Marri pia amefafanua kuwa, hadi sasa idadi kadhaa ya raia wa Qatar wametekwa nyara na Saudia na kwa ajili hiyo amewataka watawala wa Aal-Saud kuipatia majibu stahiki serikali ya Doha au kuwaachilia huru watu hao.

Bernie Sanders, Seneta wa Jimbo la Vermont nchini Marekani ambaye naye amemtaka Trump kuacha kuibeba Saudia

Katika hatua nyingine Bernie Sanders, Seneta wa Jimbo la Vermont nchini Marekani amesema kuwa, iwapo itabainika kuwa kweli Saudi Arabia ilimuua kinyama Jamal Khashoggi, mwandishi na mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud huko mjini Istanbul, Uturuki, basi Washington itatakiwa kuondoka katika ushiriki wa vita vya Riyadh nchini Yemen. Sanders ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CNN ya Marekani na kuongeza kwamba, Washington haiwezi kuendelea kuunga mkono utawala ambao kwa ujeuri unamuua mkosoaji wake ndani ya ubalozi wake.

Tags

Maoni