Oct 15, 2018 04:52 UTC
  • Wakuwait wakasirishwa na vitisho vya mwanamfalme wa Saudia dhidi ya nchi yao

Vitisho vya mwanamfalme mmoja wa Saudia juu ya uwezekano wa kutekelezwa operesheni aliyoiita kwa jina la 'Dhoruba ya Maamuzi' nchini Kuwait, vimeibua hasira ya Wakuwait.

Khalid Bin Abdullah Faisal Bin Turki Al Saud, mwanamfalme wa Saudi Arabia ameyasema hayo kupitia ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Kuwait inahitaji Dhoruba ya Maamuzi" kwa ajili ya kuwasafisha Ikhwanul Muslimin na watu wenye mafungamano na serikali ya Qatar. Kufuatia ujumbe huo, watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii nchini Kuwait wamejibu ujumbe wa mwanamfalme huyo wa Saudia, kwa kuuonya utawala wa Aal-Saud usijaribu kuingilia masuala ya ndani ya Kuwait. 'Dhoruba ya Maamuzi' ni operesheni ya muungano wa nchi za Kiarabu unaoongozwa na Saudia kwa kuungwa mkono na Marekani na utawala haramu wa Israel ambayo ilianzishwa mwezi Machi 2015 nchini Yemen, ambayo hadi sasa imepelekea zaidi ya Wayemen elfu 14 kuuawa, maelfu ya wengine kujeruhiwa na mamilioni kuwa wakimbizi.

Wafalme wa Saudia na Qatar ambao  wanatofautiana pakubwa

Raia mmoja wa Kuwait sambamba na kuzungumzia matamshi ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani aliyesema kuwa, Saudia haiwezi kusalia hai kwa muda wa wiki mbili bila ya ulinzi wa Washington, ameandika katika mtandao wa kijamii kwamba, Saudi Arabia bado inahitaji kwanza msaidizi kutoka nje kwa ajili ya kuilinda mipaka yake. Wakati huo huo, safari iliyokosa mafanikio ya Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia nchini Kuwait, imetajwa kuwa ni kushindwa kwake vibaya katika siasa za eneo kama ambavyo uhusiano wa Saudia na Kuwait ungali bado unashuhudia tofauti za kimpaka hususan tofauti zao katika vyanzo vya mafuta.

Tags

Maoni