Oct 15, 2018 07:48 UTC
  • Makampuni mengi zaidi yaisusia Saudi Arabia

Mkuu wa kampuni ya JP Morgan Chase & Co, Jamie Dimon, na mkuu wa shirika la Ford, Bill Ford ni wakuu wa karibuni zaidi wa makampuni ya Marekani waliotangaza kususia mkutano wa uwekezaji uliopangwa kufanyika nchini Saudi Arabia baadaye mwezi huu, baada ya kutoweka mwandishi anayeukosoa utawala wa Riyadh, Jamal Kahoggi katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki.

Mkuu wa kampuni ya Uber Technologies, Dara Khosrowshahi, mkuu wa shirika la Viacom, Bob Bakish na bilionea Steve Case, mmoja wa waanzilishi wa kampuni ya AOL walishatangaza mapema kuwa hawatoshiriki katika mkutano huo wa siku tatu uliopewa jina la "Davos ya Jangwani."

Siku ya Ijumaa, bilionea wa Uingereza, Richard Branson alisimamisha uhusiano wake wa kibiashara na Saudi Arabia.

Maafisa usalama wa Marekani wanasema kuwa Bin Salman amehusika katika kadhia ya Khashoggi

 

Mashirika makubwa ya habari nayo kama vile CNN, Financial Times, New York Times, CNBC na Bloomberg yamesusia mkutano huo. Shirika pekee kubwa la habari la Magharibi ambalo hadi hivi sasa halijasusia mkutano huo la Fox Business Network nalo jana lililiambisha shirika la habari la Reuters kuwa linafikiria kuangalia upya msimamo wake wa kushiriki kwenye mkutano huo.

Wimbi hili la kususiwa Saudi Arabia linaweza kuongeza mashinikizo kwa mashirika mingine ya Marekani kama vile Goldman Sachs Group Inc, Mastercad Inc na Bank of America Corp ili nayo yaangalie upya uamuzi wao wa kushiriki katika mkutano huo.

Maoni