Oct 16, 2018 03:04 UTC
  • Syria kupambana na magaidi wa Furat baada ya ushindi wa Idlib

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema vikosi vya nchi hiyo vitaelekeza nguvu na mapambano yao dhidi ya ngome za magaidi Mashariki mwa Furat, baada ya kuukomboa mkoa wa Idlib, ulioko magharibi mwa Syria.

Walid al-Muallim aliyasema hayo jana Jumatatu katika kikao na waandishi wa habari mjini Damascus, pambizoni mwa mwenzake wa Iraq, Ibrahim al-Jaafari na kusisitiza kuwa, nchi yake itaendelea kufanya kila linalowezekana kukomboa kila shibri ya ardhi yake.

Amesema mkoa wa Idlib ukishakombolewa kikamilifu, jeshi la Syria na waitifaki wake litapambana kufa kupona kukomboa eneo la Furat Mashariki, ambalo kwa sasa limedhibitiwa na wanamgambo wa Kikurdi, wanaoungwa mkono na Marekani.

Siku chache zilizopita, Rais Bashari al-Assad alisema kurejea Idlib mikononi mwa Syria kutakuwa hatari kwa mipango na njama za Marekani na Magharibi katika eneo, lakini ni lazima mkoa huo utoke kwenye makucha ya magaidi. 

Rais Assad na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq aliyeko Syria

Itakumbukwa kuwa, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (Sepah) hivi karibuni liliyashambulia makao ya viongozi wa magaidi huko mashariki mwa Furat nchini Syria kwa kutumia makombora ya balistiki ya ardhi kwa ardhi na droni kadhaa baada ya shambulizi la kigaidi la tarehe 22 Septemba huko Ahvaz kusini mwa Iran.

Katika jinai hiyo wananchi wa Iran wasio na hatia wala ulinzi  25 waliuliwa shahidi na wengine 69 kujeruhiwa.

Tags

Maoni