Oct 22, 2018 03:05 UTC
  • Kukataliwa na madola ya Magharibi simulizi za Saudia kuhusu hekaya ya mauaji ya Khashoggi

Moja ya matukio makubwa zaidi ya ukiukaji haki za binadamu kuwahi kufanywa na utawala wa Aal Saud ni la mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji maarufu wa utawala huo wa kifalme yaliyotokea ndani ya ubalozi wake mdogo ulioko mjini Istanbul, Uturuki.

Mnamo tarehe Pili Oktoba, Khashoggi alionekana akiingia kwenye jengo la ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, lakini hakuonekana tena kutoka nje ya ubalozi huo. Mauaji ya kikatili ya Jamal Khashoggi ambayo hatimaye utawala wa Aal Saud umekiri kuhusika nayo, yamelaaniwa vikali duniani na kukosolewa hata na viongozi wa nchi za Ulaya na Marekani.

Taswira ya eneo la mbele la ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki

Suala muhimu kuhusiana na mauaji hayo ni hekaya na simulizi ambazo Wasaudi wamezitoa kuhusu hatua yao hiyo ya kinyama baada ya kuandamwa na mashinikizo makubwa ya kimataifa. Mkuu wa Mashtaka wa Saudi Arabia alitoa taarifa siku ya Jumamosi ambapo mbali na kuthibitisha kuuawa kwa Khashoggi alitangaza kuwa siku hiyo ya tarehe Pili Oktoba Jamal Khashoggi alikutana na mtu mmoja ndani ya ubalozi huo mdogo wa Saudia na kwamba ati aliuawa katika mshikemshike na papatupapatu za kuingia mwilini zilizotokea kati yake na mtu huyo. Mkuu huyo wa mashtaka wa Saudia alieleleza pia katika taarifa yake hiyo kwamba, watu wanaoshukiwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi walikuwa wamekwenda Istanbul kuzungumzia uwezekano wa kumrejesha mwandishi huyo wa habari nchini Saudi Arabia.

Picha inayowaonyesha baadhi ya watu waliounda kikosi cha maafisa 15 wa Saudia wanaoaminika kutekeleza mauaji ya Jamal Khashoggi

Hata hivyo nchi nyingi duniani zinasisitiza kuwa simulizi za utawala wa Riyadh kuhusu kuuawa kwa Khashoggi zinagongana waziwazi na maelezo waliyotoa viongozi wa utawala huo hapo kabla, kwamba Jamal Khashoggi baadaye aliondoka kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul. Jamal Khashoggi alikuwa kwenye orodha ya watu wanaosakwa na utawala wa Aal Saud; na kwa sababu ya kuhofia kukamatwa aliamua kwenda kuishi nje ya Saudi Arabia. Suali la msingi linaloulizwa na wengi ni, kwa nini hapo mwanzo viongozi wa Saudia walikanusha kuwa na taarifa zozote kuhusu hatima ya raia wao huyo, lakini sasa wanakiri kwamba aliuliwa katika ugomvi wa mapigano uliotokea ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo? Lakini hata kama tutakubaliana na madai hayo ya Saudia, kuna suali la msingi zaidi linaloulizwa, ambalo ni kutaka kujua, hivi sasa mwili wa Khashoggi uko wapi na umefikwa na balaa gani? Inavyoonekana, hivi sasa utawala wa Riyadh unakabiliwa na mushkili mkubwa zaidi wa tuhuma za kuukata kata vipande vipande mwili wa Khashoggi; na inavyosemekana yumkini umezikwa kwenye maeneo ya msituni kandokando ya Istanbul. Likithibitika hilo, utawala wa Aal Saud utakumbwa na kashfa nyengine mpya ambayo hautakuwa na njia yoyote ya kujipapatua nayo.

Lakini suala muhimu linalosisitizwa na Umoja wa Ulaya na ambalo mkuu wake wa sera za nje Federica Mogherini amelitilia mkazo katika taarifa aliyotoa ni kwamba, kadhia ya mauaji ya Jamal Khashoggi inakinzana na kifungu cha 55 cha "Mkataba wa Vienna wa Uhusiano wa Kibalozi" kuhusu kuheshimu sheria za nchi mwenyeji. Hatua ya Muhammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia ya kutuma kikosi cha mauaji mjini Istanbul kilichokwenda kumtesa na kumuua kinyama Jamal Khashoggi ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia imeonyesha kuwa utawala wa Aal Saud haujali sheria wala makubaliano yoyote ya kimataifa.

Muhammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia anayeaminika kupanga mauaji ya Jamal Khashoggi

Wakati huohuo radiamali na misimamo iliyochukuliwa na viongozi wa Magharibi hasa wa nchi za Ulaya inaonyesha kuwa wao hawajaiamini hata chembe hekaya iliyosimuliwa na Wasaudi kuhusu mauaji ya Khashoggi. Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema, hakubaliani na maelezo yaliyotolewa na Riyadh kuhusu kifo cha Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari mkosoaji wa utawala wa Aal Saud. Viongozi wengine wa baadhi ya nchi za Ulaya kama Waziri Mkuu wa Denmark Lars Rasmussen, naye pia ametoa kauli inayofanana na hiyo. Maafisa wa Marekani na wabunge wa Kongresi ya nchi hiyo nao pia wametoa matamshi sawa na hayo na kusisitiza kwamba madai ya utawala wa Saudia kuhusu mauaji ya Khashoggi si ya kuaminika. Seneta Marco Rubio wa jimbo la Florida kwa tiketi ya chama tawala cha Republican amesema kuhusiana na maelezo yaliyotolewa na viongozi wa Saudi Arabia kuhusu jinsi kifo cha Khashoggi kilivyotokea, kwamba maelezo hayo ni ya kushangaza na ametaka waliohusika na mauaji hayo wawekewe vikwazo. Seneta huyo ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba: Hadithi zinazobadilika kila mara zinazotolewa na Saudi Arabia kuhusu mauaji ya Khashoggi zinaanza kuchakaa. Lazima tupige hatua mbele kwa kutumia Uchunguzi wa Kimataifa wa Magnitsky tuliouomba ili kujua nini hasa kilichotokea na kuwawekea vikwazo waliohusika. Mtazamo unaofanana na huo kuhusu kuuwekea vikwazo utawala wa Aal Saud umebainishwa pia na maafisa wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Andreas Schieder, mkuu wa kamati ya sera za nje ya Bunge la Austria ameutaka Umoja wa Ulaya uuwekee vikwazo utawala wa Saudia kutokana na mauaji ya mwandishi wa habari mkosoaji wa utawala huo. Kwa hivyo matarajio yaliyopo ni kuwaona Wamagharibi angalau wanajitoa kimasomaso kwa kuchukua za kuwawekea vikwazo baadhi ya maafisa wa Saudia. Hata hivyo kama alivyoeleza rais wa Marekani Donald Trump, vikwazo hivyo visije vikajumuisha pia uuzaji silaha kwa utawala huo wa kifalme…/

 

 

Tags

Maoni