Oct 23, 2018 06:52 UTC
  • Uri Ariel, waziri wa kilimo wa utawala wa Kizayuni wa Israel
    Uri Ariel, waziri wa kilimo wa utawala wa Kizayuni wa Israel

Waziri wa Kilimo wa utawala wa Kizayuni wa Israel usiku wa kuamkia leo ametishia kuwa, kama Jordan itataka kurejeshewa maeneo yake ya al Baqura na al Ghamr, basi Tel Aviv itaikatia maji Amman, mji mkuu wa Jordan.

Televisheni ya Rusia al Yaum imemnukuu Uri Ariel akitoa vitisho hivyo jana usiku na kuongeza kuwa, iwapo Jordan itataka kurejeshewa ardhi za al Baqura na al Ghamr, basi Tel Aviv itapunguza zaidi ya nusu ya maji yanayotumika katika mji mkuu wa Jordan, Amman.

Itakumbukwa kuwa, Mfalme Abdallah wa Pili wa Jordan juzi Jumapili alisema kuwa, muda wa mapatano ya amani yaliyotiwa saini kati ya nchi yake na Israel mwaka 1994 na hivyo Jordan kuukodisha utawala wa Kizayuni maeneo yake ya al Baqura na al Ghamr umemalizika hivyo Israel inapaswa kuirejeshea Jordan ardhi zake hizo.

Moja ya maeneo ya Jordan yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni wa Israel

 

Mwaka 1994, serikali ya kifalme ya Jordan ilitiliana saini na Israel mkataba wa amani unaojulikana kwa jina la Wadi Araba, lakini licha ya kupita miaka 25 tangu kutiwa saini mkataba huyo, hadi hivi sasa Jordan inashindwa kudhibiti maeneo yake yote.

Israel inakataa kuirejeshea Jordan maeneo yake muhimu ya kiistratijia ya al Baqura na al Ghamr yaliyoko kusini mwa Bahari Maiti au Bahari ya Chumvi (Dead Sea) na inadai kuwa maeneo hayo ni ya utawala wa Kizayuni.

Jordan ni nchi ya pili ya Kiarabu baada ya Misri kutia saini makubaliano hayo yaliyoidhinisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi baina yake na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Jordan ambayo sehemu kubwa ya wakazi wake milioni 9 ni wahajiri wa Kipalestina, ndiyo nchi yenye mpaka mrefu zaidi na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Tags

Maoni