Nov 12, 2018 07:32 UTC
  • Uwezo wa makombora ya Harakati ya Hizbullah, nukta ya nguvu ya taifa la Lebanon

Akihutubu kwa mnasaba wa 'Siku ya Shahidi' Sayyid Hassan Nasrullah ameashiria nukta ya nguvu ya Lebanon na kusema kuwa uwezo wa nchi hiyo unapatikana katika uwezo wa makombora ya muqawama na ndio maana adui hathubutu kuichokoza nchi hiyo.

Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa, usalama na amani ambayo inatawala sasa nchini Lebanon inatokana na jambo hilo na ndio maana adui anatumia njia ya vitisho na mashinikizo mbalimbali ya kidiplomasia na kuibua chuki kuhusu uwezo wa makombora hayo ya muqawama. Amesisitiza kwamba Muqawama unastafidi na fursa hiyo nzuri kwa ajili ya kulinda silaha na makombora yake. Matukio ya Lebanon yanaonyesha kwamba muhimili wa kiulinzi wa nchi hiyo unaundwa na jeshi, wananchi na muqawama katika kukabiliana na njama mbalimbali, na mhimili huo ndio alama ya mafanikio ya Lebanon kwa ajili ya kuvuka hali yoyote ya hatari. Katika uwanja huo, muqawama wa Lebanon chini ya uongozi wa Harakati ya Hizbullah na kwa uwezo wake wa makombora, ni ufunguo wa nguvu ya nchi hiyo ya Kiarabu katika nyuga tofauti. Madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani ambayo inahesabika kuwa muungaji mkono mkubwa wa utawala haramu wa Kizayuni yamekuwa yakifanya njama chafu dhidi ya uwezo wa makombora ya Hizbullah ambapo kwa kutumia visingizio tofauti, yanalenga kulizuia jeshi la nchi hiyo kuweza kujizatiti na silaha za kisasa na mifumo mipya ya makombora. Katika uwanja huo, madola hayo kwa kutumia kibri na njama tofauti hayaliruhusu jeshi la Lebanon kumiliki silaha hizo muhimu.

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon 

Nukta inayopasa kuzingatiwa ni hii kwamba, kile kinachowatia wasi wasi mkubwa maadui wa Lebanon kutokana na uwezo wa makombora ya Hizbullah, ni kwamba uwezo huo umepatikana kwa kujitegemea ambapo makombora hayo yameundwa na wanamuqawama wenyewe wa nchi hiyo. Aidha mafanikio ya muqawama katika kuvuka vizuizi vya kisiasa na kimataifa na hatimaye kutoa pigo kali dhidi ya makundi ya kigaidi na ukufurishaji na pia utawala haramu wa Kizayuni sambamba na kufelisha mradi mkubwa wa Marekani unaoitwa eti 'Mashariki ya Kati Mpya'  yameifanya Marekani na washirika wake kupatwa na kinyongo dhidi ya muqawma. Ukweli ni kwamba, Marekani ilikuwa inakusudia kutekeleza mradi wa Mashariki ya Kati Mpya na msingi wa mradi huo ulikuwa ni kuufuta kikamilifu muqawama katika muundo wa madaraka ya eneo hili. Mradi huo ulianza kutekelezwa miaka kadhaa iliyopita na utawala wa George W Bush, rais wa zamani wa Marekani kupitia Condoleezza Rice, waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa nchi hiyo katika kipindi cha vita vya siku 33 vya mwaka 2006, kati ya utawala wa Kizayuni na harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Hata hivyo kile kilichoshuhudiwa ilikuwa ni kushindwa vibaya utawala wa Kizayuni katika vita hivyo kiasi kwamba vita hivyo vilikuwa ni hujuma ya mwisho ya Israel kwa taifa la Lebanon ambapo tangu wakati huo Tel Aviv imekuwa na khofu kubwa ya kuingia katika vita vingine na harakati hiyo ya Kiislamu. Ni suala lisilo na shaka kwamba, kusimama imara muqawama katika eneo la Mashariki ya Kati, hususan nchini Lebanon, kumesasajili ushindi mkubwa dhidi ya Israel ndani ya eneo.

Moja ya mifumo ya kisasa ya makombora ya Hibullah ambayo inainyima Israel usingizi

Kuhusiana na suala hilo, Ali Faisal Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Mrengo wa Kidemokrasia kwa ajili ya Ukomboa wa Palestina anasema: "Utawala wa Kizayuni una wasi wasi mkubwa kuhusu uwezo wa kijeshi wa Hizbullah na juu ya kuanza kwa vita vyovyote vile. Kwa zana ilizonazo, Hizbullah inaweza kuisababishia hasara kubwa Israel sambamba na kusambaratisha mfumo wa ndani wa kilojestiki wa utawala huo vamizi." Mwisho wa kunukuu. Hii ni kusema kuwa, kipigo cha muqawama kilisambaratisha mfumo wa kujilinda wa utawala wa Kizayuni ambapo hata ngao ya makombora ya utawala huo ilifeli vibaya. Aidha licha ya harakati za Marekani na utawala wa Kizayuni za kuutenga muqawama katika eneo, iwe ni Palestina, Lebanon, Iraq, Syria na Yemen kupitia njama tofauti ukiwemo muamala wa karne, lakini hali ya mambo inaonyesha kwamba raia wa nchi za eneo hawapo tayari kupoteza matukufu na maslahi ya nchi zao na ni kwa msingi huo ndio maana wanautambua muqawama huo kuwa kikosi imara dhidi ya maadui wa nchi hizo. Suala hilo ndilo liliashiriwa na Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah katika maadhimisho ya Siku ya Shahidi.

Tags

Maoni