Nov 17, 2018 07:00 UTC
  • Baraza Kuu la UN lapasisha maazimio 9 dhidi ya Israel

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha maazimio 9 dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kutangaza upinzani wake dhidi ya siasa na hatua zinazochukuliwa na utawala huo.

Kamati ya Nne ya Baraza Kuu la UN imetangaza katika maazimio hayo kwamba, hatua zinazochukuliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa Palestina wanaoishi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni ukiukaji wa haki zao za kiraia. 

Maazimio hayo pia yameeleza wasiwasi wake kuhusu ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika ardhi ya Palestina, ukatili wa askari wa utawala huo dhidi ya raia na vitendo vya kichochezi vya walowezi wa Kiyahudi dhidi ya Wapalestina na kulaani vikali mienendo hiyo.

Askari wa Israel wanawaua ovyo Wapalestina.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia limeitaka Israel ikomeshe mara moja ukiukaji wa haki za binadamu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu ikiwa ni pamoja na kukomesha mauaji, kujeruhi na kuwatia nguvuni ovyo raia wasio na hatia wa Palestina.

Maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia yameitaka Israel kuheshimu azimio nambari 497 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu eneo linalokaliwa kwa mabavu la Golan na kusema Israel inapaswa kukomesha kulikalia kwa mabavu eneo hilo ambalo ni milki ya Syria.    

Tags

Maoni