Dec 09, 2018 15:05 UTC
  • Kushadidi hitilafu katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, viongozi wa Qatar na Oman hawashiriki mkutano wa Riyadh

Mkutano wa 39 wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (P)GCC unafanyika Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia bila ya kuhudhuriwa na viongozi wa Qatar na Oman, nchi mbili wanachama wa baraza hilo lenye wanachama sita.

Mkutano huo ulioanza leo huko Riyadh umegubikwa na hitilafu kubwa miongoni mwa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano ambapo mgogoro wa Qatar unatajwa kuwa chanzo kikuu cha hitilafu hizo.  

Tarehe 5 Juni mwaka uliopita wa 2017, Saudi Arabia, Imarati, Bahrain pamoja na Misri zilichukua hatua ya kuvunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar kwa sababu ya serikali ya Doha kutofuata muelekeo wa nchi za Kiarabu zinazoongozwa na Saudia. Lakini mbali na kuiwekea vikwazo Qatar, nchi hizo zilifungia pia Doha mipaka yao ya ardhini, baharini na angani.

Mnamo tarehe 23 Juni, nchi hizo nne ziliipatia Qatar orodha ya masharti 13 na kutangaza kuwa kurejeshwa tena uhusiano wa kawaida na nchi hiyo kutategemea utekelezwaji wa masharti yote hayo na serikali ya Doha.

Ramani ikionyesha zilipo nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi

Masharti muhimu zaidi ambayo Saudia na washirika wake wameishurutisha Qatar ni kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran na Hizbullah ya Lebanon, kuifunga stesheni ya televisheni ya Aljazeera na kuondoa kituo cha kijeshi cha Uturuki ndani ya ardhi ya Qatar. Serikali ya Doha imeyakataa masharti hayo.

Kutoshiriki Sultan Qaboos bin Said wa Oman na Amir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani katika mkutano wa Baraza la Ushirikkiano la Ghuba ya Uajemi huko Riyadh hasa katika kipindi hiki nyeti, kunaonyesha kushadidi hitilafu miongoni mwa nchi wanachama wa baraza hilo.

Maoni