Dec 09, 2018 15:11 UTC
  • Hizbullah: Hakuna hata sehemu moja ya Israel itakayosalimika na makombora yetu

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, hakuna hata sehemu moja ya Israel ambayo haiwezi kufikiwa na makombora ya harakati hiyo ya muqawama.

Sheikh Naim Qassem ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la al-Vefagh linalochapishwa mjini Tehran na kufafanua kuwa: "Hakuna hata sehemu moja ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu isiyoweza kufikiwa na makombora ya Hizbullah."

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeshawahi kufanya uvamizi na hujuma kadhaa za kijeshi katika mpaka wake wa pamoja na Lebanon, na hivi karibuni waziri mmoja wa utawala huo ghasibu alidokeza kuhusu uwezekano wa kuivamia tena Lebanon kwa lengo la kubomoa kile alichodai kuwa ni njia za chini kwa chini zilizochimbwa na Hizbullah.

Kuhusiana na vitisho hivyo, Sheikh Naim Qassem amesema: "Wazayuni hawawezi kuhimili hatari kubwa kama hiyo kwa kutaka kupambana na Hizbullah, na ndiyo maana hawana mori wa kuingia katika vita vingine na Lebanon."

Ameongeza kuwa, harakati hiyo ya muqawama ya Lebanon imejizatiti kwa kinga ya ulinzi ambayo imeifanya Israel isithubutu kuanzisha chokochoko dhidi ya Lebanon tangu baada ya vita vya mwaka 2006.

Wanamuqawama wa Hizbullah wakifyatua makombora kuelekea Israel 

"Hata wanapotoa vitisho huwa wanasema, 'ikiwa Hizbullah itatushambulia' tutajibu mapigo, kwa sababu mikakati iliyowekwa na Hizbullah ndani ya Lebaon imeifanya Israel iiwiye vigumu mno hata kujiwa na wazo la kuanzisha vita dhidi ya Lebanon", amesisitiza Sheikh Naim Qassem.

Wiki iliyopita utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha kile ulichokipa jina la "Operesheni ya Ngao ya Kaskazini" ya eti kufichua na kubomoa njia za chini kwa chini zilizochimbwa na Hizbullah kuelekea ndani ya Israel.

Waziri wa Intelijensia na Usafiri wa utawala huo Yisrael Katz alitamka siku ya Ijumaa kwamba, huenda ikahitajika vikosi vya jeshi la Israel viingie ndani ya ardhi ya Lebanon kwa ajili ya kuzishughulikia njia hizo.

Endapo utawala wa Kizayuni wa Israel utaanzisha uchokozi na uvamizi dhidi ya Lebanon utaibua moto mkali wa makabiliano makali kati yake na Hizbullah.

Harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu nchini Lebanon imeshaonya kuwa utawala huo haramu "utajuta" endapo utaivamia nchi hiyo.../ 

Tags

Maoni