Dec 12, 2018 16:19 UTC
  • Hamas: Israel ndiyo itakayobeba lawama za lolote baya litakalomtokea Mahmoud Abbas

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ndio utakaobeba jukumu na lawama za jambo lolote baya litakalomtokea Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Msemaji wa HAMAS, Fauzi Barhoum amesema hayo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, kitendo cha utawala wa Kizayuni cha kutishia hadharani kuwa utamuua Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, kinaonesha jinsi utawala huo dhalimu ulivyosimama juu ya msingi wa udhalimu na kumwaga damu za watu. 

Jana Jumanne baadhi ya Wazayuni walisambamba vipeperushi na kubandika matangazo katika vituo vya upekuzi vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wakichochea kuuliwa kigaidi Mahmoud Abbas.

Fauzi Barhoum

 

Siku ya Jumatatu, Rais huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alilaani madai kwamba eti Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ni kundi la kigaidi na kusisitiza kuwa, taifa la Palestina kamwe haliutambui "Muamala wa Karne" na litaendelea kusimama kidete kupigania haki zake.

Wakati huo huo Saib Uraiqat, Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO ametoa tamko na kuitaka jamii ya kimataifa na nchi zote duniani kulaani uchochezi wa utawala wa Kizayuni wa kutaka kuuliwa kigaidi Mahmoud Abbas na kuyataka mataifa ya dunia yasimame kupinga siasa za Israel za kuvunja sheria za kimataifa na jinai nyingine zinazotendwa na utawala huo katili.

Tags

Maoni