Dec 13, 2018 10:56 UTC
  • Mashambulio ya nje ya mipaka, mwaka mmoja tangu kusambaratishwa DAESH (ISIS) nchini Iraq

Ndege za kivita za Iraq siku ya Jumanne ya tarehe 11 Desemba zilishambulia ngome mbili za kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) katika mkoa wa Deir ez-Zor nchini Syria na kuwaangamiza na kuwajeruhi makumi ya makamanda na wapiganaji wa kundi hilo la ukufurishaji.

Operesheni hiyo ya ndege za kivita za Iraq ilitekelezwa sambamba na kutimia mwaka mmoja tangu kundi la kigaidi la Daesh liliposambaratishwa nchini Iraq. Tarehe 10 Desemba katika kalenda ya Iraq imepewa jina la siku ya "Kukombolewa Kikamilifu Iraq kwa Kuondolewa Uchafu wa DAESH."

Aliyekuwa waziri mkuu wa Iraq Haidar al Abadi (aliyeshika bendera kwa mkono wa kulia) akitangaza ushindi wa Iraq dhidi ya DAESH (ISIS)

Kwa usaliti na uhaini uliofanywa na baadhi ya vibaraka wa ndani, na kwa msaada na uungaji mkono wa baadhi ya nchi za nje, mnamo mwezi Juni 2014, kundi la Daesh lilifanikiwa kuingia ndani ya ardhi ya Iraq na baadaye kukalia thuluthi moja ya ardhi yote ya nchi hiyo.

Kuwepo kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji ndani ya ardhi ya Iraq kulidumu kwa muda wa miaka mitatu na nusu, lakini athari za liliyoyafanya katika kipindi cha kuwepo kwake, kamwe hazitafutika katika fikra za wananchi wa nchi hiyo. Katika muda huo wa kuwepo "jinamizi" la Daesh nchini Iraq, maelfu ya raia waliuawa na kujeruhiwa na mamilioni ya Wairaqi wengine walibaki bila makazi. Zaidi ya hayo, wanawake wengi walibakwa, miundomsingi ya maisha hususan ya kilimo iliteketezwa; na kwa ujumla, hali ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ya Iraq ilivurugwa. Hakuna shaka kuwa, kama si fatwa ya kihistoria iliyotolewa na Marjaa Taqlidi wa nchi hiyo na misaada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kundi la kigaidi la Daesh hadi leo lingelikuwa limepiga kambi ndani ya ardhi ya Iraq.

Ayatullah Ali Sistani, Marjaa Taqlidi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq

Baada ya Daesh kuvamia na kuyakalia maeneo mengi ya ardhi ya Iraq, Sheikh Mahdi Karbalai, mwakilishi wa Ayatullah Ali Sistani, fakihi mkuu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq alitangaza katika hotuba za Sala ya Ijumaa kwamba: "Ni wajibu kwa raia wote wenye uwezo wa kubeba silaha kulinda nchi, taifa na matukufu yao na kujiunga na vikosi vya usalama kwa njia ya kujitolea ili kutekeleza jukumu hilo takatifu." Matunda ya fatwa hiyo ya kihistoria yalikuwa ni kuundwa harakati ya Hashdu-Sha'abi nchini Iraq, ambayo ilitoa mchango mkubwa sana katika kupambana na ugaidi wa Daesh. Katika wakati huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ilikuwa nchi pekee, ambayo kwa ombi la serikali ya Iraq, ilishiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ugaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh na ikatoa mchango muhimu katika kulitokomeza genge hilo ndani ya ardhi ya nchi hiyo.

Wapiganaji wa kujitolea wa harakati ya Hashdu-Sha'abi

Kwa kuzingatia kuwa umepita mwaka mmoja sasa tangu kuyoyoma ndoto ya kusimamishwa 'ukhalifa' wa Daesh nchini Iraq, suali la kujiuliza ni, kundi hilo la kigaidi liko katika hali gani hivi sasa nchini humo?

Hali halisi katika medani za vita na ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa mizizi ya kundi la Daesh imeshang'olewa nchini Iraq na wala hakuna tena 'dola' la kundi hilo nchini humo, lakini mabaki ya Daesh yamesalia katika baadhi ya maeneo ya kijiografia ya Iraq yakijaribu kama ilivyokuwa kuanzia mwaka 2014 kufanya operesheni za kigaidi na hujuma za kuripua kwa mabomu maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Michael Knights, mtaalamu wa masuala ya Iraq katika taasisi ya "Mashariki ya Karibu" iliyoko mjini Washington, Marekani anaizungumzia hali hiyo kwa kusema: "Madaesh wanakuchukulia kupoteza miji ya asili waliyokuwa wakiidhibiti nchini Iraq, kuwa ni sawa na kupoteza moja tu ya maeneo kadhaa katika vita vya muda mrefu walivyoanzisha; na wala hawaliangalii hilo kama mwisho wa operesheni zao, bali wanalitazama kama harakati mojawapo kwa ajili ya kuingia katika awamu mpya ya operesheni zao hizo."

Michael Knights

Kuhusiana na nukta hiyohiyo, mnamo mwezi Septemba mwaka huu, gazeti la The Atlantic, linalochapishwa nchini Marekani lilitoa ripoti kwa anuani ya "Mustakabali wa Daesh nchini Iraq" inayoeleza kwamba: "Moja ya ishara muhimu ya kuonyesha kuwa Daesh inao uwezo wa kurudi na kujitokeza tena, ni wakuu kadhaa wa makabila waliouliwa na kundi hilo. Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, kwa wastani wa kila wiki wazee na wakuu watatu wa kikabila waliuliwa na kundi la Daesh; na tangu mwaka uliopita hadi sasa, karibu vijiji 200 vimeshuhudia kuuawa kwa wazee na wakuu wao wa kikabila."

Mji wa Kirkuk, baada ya kukombolewa kutoka kwenye makucha ya DAESH

Inavyoonyesha, ni kutokana na uwezo huo, ndipo serikali na jeshi la Iraq zikafikia uamuzi kwamba, ili kuvunja kikamilifu au angalau kudhoofisha uwezo wa Daesh na kwa njia hiyo kulizuia lisirejee tena ndani ya ardhi ya Iraq, kuna ulazima wa kuendeleza mapambano dhidi ya kundi hilo la kigaidi nje ya nchi hiyo, hususan katika ardhi ya Syria. Kwa hakika hatua iliyochukuliwa siku ya Jumanne na ndege za kivita za Iraq ya kushambulia ngome za Daesh nchini Syria, tunaweza kuitaja kama "shambulio la nje ya mipaka" ya Iraq dhidi ya Daesh kwa lengo la kutokomeza nguvu na uwezo wa kurudi tena genge hilo la kigaidi na ukufurishaji ndani ya ardhi ya nchi hiyo.../ 

Maoni