Dec 14, 2018 06:31 UTC
  • Malengo ya Saudi Arabia ya kuanzisha mfumo maalumu wa kisheria wa nchi za Bahari Nyekundu

Serikali ya ukoo wa Aal Saud ya nchini Saudi Arabia imetangaza habari ya kuanzishwa mfumo maalumu wa kisheria wa nchi za Bahari Nyekundu.

Bahari nyekundu ni eneo muhimu sana la kibiashara na kiuchumi kwa nchi zinazopakana nalo. Umuhimu wa Bahari Nyekundu unaongezeka kutokana na kwamba bahari hiyo inaungana na Bahari ya Mediterranean kupitia Mfereji wa Suez na kwa upande wa pili inaungana na lango bahari la Bab al Mandab na Ghuba ya Aden na kufika hadi kwenye Bahari ya Hindi. 

Zaidi ya hayo ni kwamba, asilimia 15 ya biashara ya dunia inategemea Bahari Nyekundu. Ni kwa kuzingatia jambo hilo, ndio maana mkutano wa kwanza wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu na Kiafrika zinazopakana na Bahari Nyekundu ulifayika tarehe 12 Disemba 2018 katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh ukishirikisha nchi saba. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, juhudi za Saudia za kuanzisha muungano huo ni kukabiliana na washindani wake katika eneo hilo hususan Uturuki. Hasa kwa kuzingatia kuwa hivi karibuni Sudan ambayo ni moja ya nchi zinazopakana na Bahari Nyekundu, iliipa Uturuki zabuni ya kukiendeleza kisiwa cha Sawakin cha Bahari Nyekundi. Wachambuzi hao wanasema kuwa, kwa hakika Saudi Arabia inafanya juhudi za kuzizuia nchi zinazopakana na Bahari Nyekundu zisiende upande wa washindani wa Riyadh.

Mipaka ya Bahari Nyekundu

 

Kwa kuzingatia kuwa nchi nyingi ziinazopakana na Bahari Nyekundu zina matatizo ya kifedha na zinaitegemea Saudia kudhamini mahitaji yao hayo, ukoo wa Aal Saud umeamua kuzuia ushawishi wa nchi nyingine katika eneo hilo kama vile Uturuki kupitia kuanzisha mfumo maalumu wa kisheria wa Bahari Nyekundu.

Suala jingine ni kwamba kupitia kuanzisha mfumo huo maalumu wa kisheria, Saudi Arabia inajaribu kukabiliana na ushawishi unaozidi kuongezeka wa nchi ndogo ya Qatar katika nchi zinazopakana na Bahari Nyekundu. Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita na hasa kipindi cha miezi 18 nyuma, Qatar imewekeza mno katika nchi zinazopakana na Bahari Nyekundu, hivyo hivi sasa Saudia inaonekana kwa namna fulani inataka kukabiliana na uwekezaji huo mkubwa wa vitega uchumi wa Doha.

Nukta nyingine ni kwamba, hatua ya Saudi Arabia ya kuanzisha mfumo maalumu wa kisheria wa nchi za Bahari Nyekundu ni kujaribu kutia nguvu kampeni ya ukoo wa Aal Saud ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na juhudi zake za kuupa utawala huo khabithi nafasi ya kutumia itakavyo eneo la Bahari Nyekundu.

Nchi zinazopakana na Bahari Nyekundu

 

Gazeti la nchini Qatar la al 'Arabi al Jadid limeandika: "Kwa kuzingatia umuhimu wa Israel kuwa na mkono katika eneo la Bahari Nyekundu, kuundwa muungano huo kunaweza kuwa ni hatua ya siri ya kujaribu kuzifanya nchi zote za fukwe za bahari hiyo ziwe na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni."

Tunaweza kusema kuwa, ingawa Israel haikushiriki rasmi katika kikao cha tarehe 12 Disemba 2018 cha mjini Riyadha cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zinazopakana na Bahari Nyekundu, lakini Tel Aviv inafurahishwa sana na hatua ya Saudia ya kuanzisha muungano kama huo. 

Ukitoa nchi za Saudi Arabia, Misri, Sudan, Djibouti, Yemen, Somalia na Jordan zilizoshiriki kwenye kikao hicho cha Riyadh, Eritrea nayo inapakana na Bahari Nyekundu pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel. Kutoshiriki Eritrea kwenye kikao cha Riyadh ni uthibitisho kuwa kuanzisha muungano huo hakujapata ridhaa ya nchi zote zinazopakana na Bahari Nyekundu. Vile vile mivutano iliyopo baina ya Sudan na Saudi Arabia hasa kutokana na msimamo wa Khartoum wa kuimarisha uhusiano wake na nchi kama za Qatar na Uturuki ni ushahidi mwingine wa kwamba Saudi Arabia haitoweza kufikia kikamilifu malengo yake. 

Jambo jingine muhimu ni kwamba, Marekani, China, Japan, Ufaransa, Uturuki na Israel zina vituo vyao vya kijeshi katika fukwe za Bahari Nyekundu. Hivyo nchi zinazopakana na bahari hiyo lazima zitilie maanani manufaa ya nchi hizo. 

Nukta nyingine muhimu ni kwamba, licha ya kuwa Saudia imesema kwenye kikao cha tarehe 12 Disemba huko Riyadh kwamba moja ya malengo ya kuanzishwa muungano huo ni kudhamini usalama wa Bahari Nyekundu lakini ni hiyo hiyo Saudia kwa kushirikiana na wavamizi wenzake wa Yemen ndiyo inayoendelea kuhatarisha usalama wa eneo hilo kutokana na vita vya pande zote ilivyovianzisha dhidi ya wananchi maskini wa Yemen tangu miezi 45 iliyopita.

Tags

Maoni