Dec 15, 2018 06:25 UTC
  • Wasiwasi wa kuongezeka misaada ya Magharibi kwa magaidi wa Syria

Tangu mwaka 2011 yalipoanzishwa machafuko nchini Syria hadi hivi sasa, nchi za Magharibi hasa Marekani, Uingereza na Ufaransa pamoja na vibaraka wao baadhi ya nchi za Kiarabu zimekuwa zikiyaunga mkono kwa hali na mali magenge ya kigaidi kwa tamaa ya kuipindua serikali iliyoko madarakani kihalali nchini Syria.

Hata hivyo kutokana na ushindi mkubwa lilioupata jeshi la Syria na waitifaki wake na kushindwa mtawalia magenge ya kigaidi, hivi sasa madola ya kibeberu na vibaraka wao yanahisi kwamba ndoto zao zimekwenda na upepo na ndio maana zinatumia visingizio vya kila namna kujaribu kuidhoofisha Damascus kwa namna nyingine. 

Nchi za Magharibi sasa zinataka kulitumia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupasisha azimio la kuingilia masuala ya ndani ya Syria kwa kisingizio cha kutoa misaada katika mipaka ya nchi hiyo. Hata hivyo njama hizo zimekataliwa na waungaji mkono wa taifa la Syria na ndio maana juzi Alkhamisi nchi za Russia na China zilipinga njama hizo za Magharibi za kujaribu kuwafikishia misaada magaidi wa Syria kwa madai ya uongo ya eti kuwasaidia wananchi wa Syria kupitia mipaka ya nchi kavu.

Wanajeshi vamizi wa Marekani ndani ya ardhi ya Syria

 

Tangu mwaka 2014 hadi hivi sasa Baraza la Usalama limekuwa ikichukua natua mbalimbali za kupeleka misaada katika maeneo yanayodhibitiwa na magaidi kupitia mipaka ya Uturuki, Iraq na Jordan bila ya idhini ya serikali ya Syria na licha ya onyo linalotolewa mara zote na Damascus kwamba huko ni kuvunja haki ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu. Baada ya Sweden na Kuwait kuwasilisha pendekezo hilo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia, mwakilishi wa Russia katika umoja huo amesema kuwa, mpango huo si sahihi na hauzingatii uhalisia wa mambo. Amesema, serikali ya Syria ndiyo yenye haki ya kuwafikishia misaada raia wake na tayari kuna kivuko kimetengwa na serikali ya Damascus kuhusu jambo hilo. Vile vile amesema, utulivu unazidi kuongezeka nchini Syria hivi sasa licha ya kuweko matatizo mengineyo na hadi hivi sasa kumeshachukuliwa hatua nyingi na serikali za kuboresha hali ya kibinadamu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Hivyo Moscow inaamini kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kufikisha misaada hiyo kupitia kwa serikali ya Syria na sio kutumia kisingizio cha misaada ya kibinadamu kuwafikishia misaada ya kijeshi magaidi wanaofanya jinai za kila namna nchini humo.

Msimamo huo wa Russia umeungwa mkono pia na China ambayo nayo ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ma Zhaoxu, mwakilishi wa China katika umoja huo amesema kuwa, operesheni ya kufikisha misaada kwa wahitaji nchini Syria inapaswa kufanyika kwa ungalifu mkubwa na kutopendelea upande wowote na wala kusiingizwe siasa katika jambo hilo kama ambavyo ni wajibu pia ifanyike kwa idhini na uangalizi wa serikali iliyoko madarakani kihalali huko Syria. China ni moja ya madola matano yenye haki ya veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Russia nayo ina haki ya kura ya veto katika baraza hilo. Hatua ya China ya kutangaza waziwazi uungaji mkono wake kwa serikali ya Rais Bashar al Assad ya Syria inapunguza uwezekano wa kufanikiwa njama za madola ya Magharibi yasiyowapendea kheri wananchi wa nchi hiyo waliotumbukizwa kwenye masaibu makubwa na madola hayo hayo ya Magharibi. 

Ma Zhaoxu, mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa

 

Wachambuzi wa mambo wanasema wazi kuwa, lengo hasa la nchi za Magharibi ni kuwafikishia misaada ya kilojistiki magaidi waliozingirwa na kudhoofishwa sana na serikali ya Syria. Madola hayo ya kibeberu na vibaraka wao yanatumia kisingizio cha misaada ya kibinadamu kuficha njama zao hizo. Lakini njama zao hizo zimegunduliwa na ni kama alivyosema Aaron Lund, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Sweden kwamba, kwa upande wa kiistratijia, Rais Bashari al Assad wa Syria ameweza kuwashinda maadui zake ambao kwa miaka mingi sasa wanafanya njama za kuipindua serikali yake.

Tags

Maoni