Dec 15, 2018 07:35 UTC
  • Ndege za kivita za Saudia zaishambulia Hudaydah licha ya mapatano

Ndege za kivita za Saudi Arabia zimeshambulia kwa mabomu mji wa al-Hudaydah, siku moja baada ya kufikiwa mapatano baina ya pande mbili nchini Yemen, kufuatia mazungumzo yaliyohusu mji huo wa bandari wa magharibi mwa nchi yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Mkazi wa mji huo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, binafsi alisikia sauti za makombora na risasi jana Ijumaa katika kijiji cha Julai 7, mashariki mwa al-Hudaydah.

Kanali ya televisheni ya al-Masirah imeripoti kuwa, ndege za kijeshi za Saudia zimefanya mashambulizi mawili ya anga katika mji wa Ras Isa, kaskazini mwa Hudaydah.

Bandari ya Hudaydah

Siku ya Alkhamisi mwakilishi wa Harakati ya Ansarullah katika mazungumzo ya Sweden alitangaza kuwa pande mbili zimeafikiana kuhusu usitishwaji mapigano katika bandari ya Al Hudaydah.

Duru ya kwanza ya mazungumzo hayo ilianza Disemba 6 na kumalizika Disemba 13 nchini Sweden. Utawala wa zamani wa Yemen unaoungwa mkono kikamilifu na Saudia ndio uliokuwa upande ya pili katika mazungumzo hayo yaliyofanyika chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa.

Martin Griffiths, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa jana Ijumaa aililiambia Baraza la Usalama kuwa pande mbili za Yemen zinatazamiwa kuondoka katika mji huo bandari ndani ya siku chache zijazo.

Tags

Maoni