Dec 15, 2018 12:15 UTC
  • Safari ya Waziri Mkuu wa Tunisia nchini Saudi Arabia na malengo yake

Waziri Mkuu wa Tunisia, Youssef Chahed Alkhamisi iliyopita aliwasili Riyadh akiwa katika safari ya siku tatu ya kuitembelea Saudi Arabia.

Katika miaka ya hivi karibuni uhusiano wa Riyadh na Tunis umekuwa na panda shuka nyingi. Saudi Arabia ilikuwa miongoni mwa wapinzani wakuu wa mapinduzi ya wananchi wa Tunisia mwaka 2011 dhidi ya utawala wa dikteta wa zamani wa nchi hiyo Zainul Abidin bin Ali aliyekimbilia Riyadh baada ya kung'olewa madarakani. Tangu wakati huo vyombo vya sheria vya Tunisia na wananchi wa nchi hiyo walitaka dikteta huyo arejeshwe nchini na kupandishwa kizimbani lakini Saudia imekataa ombi hilo.

Dikteta wa zamani wa Tunisia, Zainul Abidin amepewa hifadhi Saudi Arabia.

Suala jingine ni kwamba, katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Tunisia ilikuwa miongoni mwa wakosoaji wa siasa za nje za Saudi Arabia hususan kuhusu mgogoro wa Syria. Sambamba na kupinga uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya Syria, Tunisia daima imekuwa ikisisitiza udharura wa kuanzishwa tena uhusiano nzuri na serikali ya Damascus. Suala hilo kwa upande mwingine linapingana na stratijia za serikali ya Riyadh. 

Wakati huo huo Saudia imekuwa ikifuatilia kwa makini masuala ya ndani ya Tunisia na imefanya jitihada kubwa za kumrejesha madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Zainul Abidin bin Ali au kuwasimika madarakani watu wenye uhusiano wa karibu na watawala wa Riyadh. Katika uwanja huo Jouhar bin Mubarak ambaye mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Tunisia anasema: "Mwanzoni mwa mwaka huu Saudi Arabia ikishirikiana na Imarati zimefanya jitihada kubwa za kumsaidia waziri wa zamani wa mambo ya ndani wa Tunisia, Lotfi Brahem kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya sasa ya nchi hiyo. Safari iliyofanywa na Lotfi Brahem nchini Saudi Arabia mwanzoni mwa mwaka huu wa 2018 ambayo hatimaye ilikuwa sababu ya kutimuliwa madarakani pia ilikuwa sehemu ya mpango wa mapinduzi wa Saudia na Imarati dhidi ya serikali ya sasa ya Tunisia."

Lotfi Brahem nchini Saudia

Mfichuaji wa siri za ndani ya utawala wa Saudia maarufu kwa jina la Mujtahid anasema: "Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lotfi Brahem alikuwa kamanda wa Gadi ya Taifa ya Kupambana na Ugaidi nchini Tunisia. Kwa msingi huo watawala wa kifalme wa Saudia walikuwa na matumaini makubwa kwamba, kwa njia hiyo wataweza kumrejesha madarakani dikteta Zainul Abidin bin Ali."

Kwa kutilia maanani hayo yote kunajitokeza swali kwamba, safari ya Youssef Chahed nchini Tunisia inafanyika kwa malengo gani?

Inaonekana kuwa, lengo kuu zaidi la safari hiyo linafungamana na hali ya kiuchumi ya Tunisia. Kwa sasa serikali ya nchi hiyo inasumbuliwa na matatizo mengi hususan yale ya kiuchumi, na kutokana na hali hiyo hivi karibuni kumejitokeza harakati ya "visibao vyekundu" inayofuata nyayo za vuguvugu la "visibao vya njano" nchini Ufaransa. Harakati ya visibao vyekundu imeundwa kupinga matatizo ya kiuchumi ya Tunisia ikiwa ni pamoja na ughali wa bidhaa na maisha, ukosefu mkubwa wa ajira na sera zisizo sahihi za kiuchumi za serikali ya nchi hiyo.

Itakumbukwa kuwa, katika safari yake ya masaa matatu tu nchini Tunisia hapo tarehe 27 Novemba, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia Muhammad bin Salman aliahidi kuipatia nchi hiyo msaada wa dola bilioni mbili na kuwekeza katika miundombinu ya nchi hiyo. Inaonekana kuwa safari ya Waziri Mkuu wa Tunisia nchini Saudi Arabia inafanyika kufuatilia ahadi hiyo ya Muhammad bin Salman.

 Youssef Chahed na Mfalme Salman wa Saudi Arabia

Mbali na hayo mwaka ujao wa 2019 Tunisia itashuhudia chaguzi za rais na bunge. Hivyo Youssef Chahed ambaye ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu kutoka chama cha Nidaa Tounes ambaye pia ni mkwe wa Rais Beji Caid Essebsi wa nchi hiyo, anafanya mikakati ya kupata misaada ya kifedha na msaada wa vyombo vya habari vya utawala wa Aal Saudi au vinavyofadhiliwa na utawala wa Riyadh kwa ajili ya kukabiliana na chama cha Kiislamu cha al Nahdha katika uchaguzi wa mwaka ujao. Chama hicho ndio mpinzani mkubwa zaidi wa utawala wa sasa wa Tunisia.      

Maoni