Dec 15, 2018 14:30 UTC
  • Saudia imekiuka mapatano ya Hudaydah, Yemen mara 21 masaa 24 yaliyopita

Saudi Arabia imekiuka mapatano ya amani ya Yemen kwa kutuma ndege zake za kivita kushambulia eneo la Hudaydah mara 21 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.

Msemaji wa Jeshi la Yemen Brigedia Yahya Sare'e ameiambia Televisheni ya Al Masira kuwa ndege za kivita za Saudia zimevurumisha makombora katika maeneo ya raia mkoani Hudaydah na hivyo kukiuka mapatano ya usitishaji vita yaliyofikiwa Alhamisi.

Aidha Brigedia Sare'e amesema mamluki wa Saudia walijaribu kujipenyeza Hudaydah kwa kutumia pwani ya magharibi mwa Bahari ya Sham lakini wapiganaji wa Yemen waliwazuia. Msemaji huyo wa Jeshi la Yemen amesisitiza kuwa wako tayari kuandaa mazingira ya kufanikisha mapatano ya amani ili kuwapunguzia Wayemen masaibu waliyonayo lakini akaongeza kuwa wako tayari pia kukabiliana na adui atakayekiuka mapatano hayo.

Siku ya Alkhamisi mwakilishi wa Harakati ya Ansarullah katika mazungumzo ya Sweden alitangaza kuwa pande mbili zimeafikiana kuhusu usitishwaji mapigano katika bandari ya Al Hudaydah.

Bandari ya Hudaydah ina umuhimu mkubwa hasa katika kuwafikishia Wayemen misaada ya dharura

Duru ya kwanza ya mazungumzo hayo ilianza Disemba 6 na kumalizika Disemba 13 nchini Sweden. Utawala wa zamani wa Yemen unaoungwa mkono kikamilifu na Saudia ndio uliokuwa upande wa pili katika mazungumzo hayo yaliyofanyika chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa.

Martin Griffiths, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa jana Ijumaa aliliambia Baraza la Usalama kuwa pande mbili za Yemen zinatazamiwa kuondoka katika mji huo wa bandari ndani ya siku chache zijazo.

 

Tags

Maoni