Dec 16, 2018 08:09 UTC
  • Mkutano wa kimataifa wa Doha 2018, uasi wa Qatar dhidi ya Saudia

Katika kipindi cha chini ya wiki moja baada ya mkutano wa 39 wa viongozi wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemu uliofanyika Riyadh nchini Saudi Arabia, Qatar imeitisha mkutano wa kimataifa ulioanza jana mjini Doha ukihudhuriwa na watu mashuhuri akiwemo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Muhammad Javad Zarif.

Mkutano wa siku mbili wa kimataifa wa Doha 2018 kwa sababu moja au nyingine unaweza kutambuliwa kuwa ni kielelezo cha azma kubwa ya Qatar ya kukabiliana na sera za kibeberu za Saudi Arabia.

Sababu ya kwanza kabisa ni kuhusiana na kiwango cha ushiriki na vyeo na nafasi za watu mashuhuri wanaoshiriki mkutano wa Doha 2018 ikilinganishwa na wale walioshiriki mkutano wa viongozi wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi mjini Riyadhi wiki iliyopita. Mkutano wa Riyadh ulihudhuriwa na viongozi wa nchi tatu tu za Saudi Arabia iliyokuwa mwenyeji, Kuwait na Bahrain; viongozi wa Qatar, Oman na Imarati hawakuhudhuria mkutano huo. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, ushiriki ulikuwa wa chini na mdogo katika mkutano wa Riyadh na kwa sababu hiyo kuna tetesi za uwezakano wa kusambaratika Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (PGCC). Hali hii imetambuliwa kuwa ni ushindi na goli la kisigino la Qatar dhidi ya Saudi Arabia.

Muhammad Javad Zarif

Mbali na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Mkutano wa Doha 2018 unahudhuriwa na watu mashuhuri kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa María Fernanda Espinosa Garcés, mawaziri wa mambo ya nje wa Uturuki na Oman, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Nadia Murad na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia. Kwa msingi huu tunaweza kusema kuwa, kwa mkutano huu, Qatar imefanikiwa kutoa pigo la kidiplomasia kwa Saudia inayoendelea kuandamwa na fikra za walimwengu na imewaonesha viongozi wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo kwamba, mkutano wa wiki iliyopita mjini Riyadh haukuwa na umuhimu wowote kwa viongozi wa Doha. 

Mkutano wa Doha 2018

Sababu ya pili inahusiana na matamshi ya Amir wa Qatar na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo katika mkutano wa Doha 2018. Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani amekariri tena msimamo wa nchi yake kuhusu mgogoro na nchi nne za Saudia, Bahrain, Imarati na Misri na kusema, utatuzi wa mgogoro huo unawezekana kupitia njia ya mazungumzo na kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Pamoja na hayo matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Muhammad bin Abdur Rahman Aal Thani katika mkutano wa Doha 2018 yanatambuliwa kuwa ni aina fulani ya uasi dhidi ya Saudi Arabia. Muhammad bin Abdur Rahman Aal Thani amekosoa utendaji wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi na kulitaja kuwa ni baraza lililofeli na kushindwa. Vilevile ametoa wito wa kuarifishwa tena miungano na jumuiya za kieneo na kikanda.

Japokuwa Amir na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar hawakutaja jina la Saudi Arabia moja kwa moja lakini ishara walizotoa zinaelekea moja kwa moja kwa Saudi Arabia hususan pale Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar aliposema: "Suala la kurejeshwa uhusiano linapaswa kuambatana na kuheshimiwa haki ya kujitawala."

Doha

Matamshi ya Amir na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar katika mkutano wa Doha 2018 na kususia kwao wa mkutano wa wiki iliyopita wa Riyadh ambao ulipata pigo la kutohudhuriwa na nusu ya wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (PGCC) ni ishara kwamba, baada ya kujiondoa katika jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta ya OPEC sasa Qatar inajitayarisha kuondoka katika barazala la PGCC na hivyo kukata kabisa mirija yote ya udhibiti na ushawishi wa Riyadh nchini Qatar.   

Maoni