Dec 16, 2018 15:18 UTC
  • Jeshi la anga la Iraq lafanya oparesheni dhidi ya Daesh katika ardhi ya Syria

Wanamgambo kadhaa wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh wameangamizwa katika shambulio la anga la jeshi la Iraq lililolenga mkusanyiko wa viongozi wa Daesh katika eneo la al Susah mkoani Deir Zor nchini Syria.

Abu Ali al  Basri, Mkuu wa Idara ya Habari na Kupambana na Ugaidi nchini Iraq amesema kuwa magaidi wa Daesh walikuwa na lengo la kuingia katika ardhi ya Iraq na kwamba miongoni mwa magaidi waliouliwa ni Anad al Muhammadi, Waziri wa Vita wa Daesh na Sajjad Ali Hussein al Hasnawi, naibu wa Abubakar al Baghdadi, kiongozi mkuu wa genge hilo. 

Abu Bakar al Baghdadi, aliyejitangaza kuwa kiongozi wa kundi la Daesh

Kituo cha upashaji habari cha kamandi ya jeshi la Iraq Jumanne tarehe 11 Disemba pia kilitangaza habari ya kushambuliwa ngome za kundi la Daesh katika mkoa wa Deir Zor mashariki mwa Syria. Ndege za kivita aina ya F-16 za Iraq ndizo zilizotekeleza mashambulio hayo dhidi ya Daesh na kuuwa magaidi kadhaa. Kabla ya mashambulio haya tajwa, ndege za kivita za Iraq zilikuwa zimetekeleza oparesheni kadhaa dhidi ya maeneo ya kundi la Daesh katika ardhi ya Syria kwa kushirikiana na serikali ya nchi hiyo. 

Pamoja na kuwa kundi la kigaidi la Daesh limepata kipigo kikali huko Iraq na Syria, lakini mamluki waliosalia wa kundi hilo wangali wametapakaa katika maeneo ya katikati mwa Iraq na Syria na wanaendelea kufanya hujuma za kigaidi katika maeneo hayo.   

 

Tags

Maoni