Dec 17, 2018 04:06 UTC
  • Rais wa Sudan awa kiongozi wa mwanzo wa Arab League kuitembelea Syria miaka 8 tangu vilipoanza vita

Rais Omar al-Bashir wa Sudan amefanya safari nchini Syria na kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) kuitembelea nchi hiyo tangu ulipoanza mgogoro wa ndani miaka minane iliyopita.

Al-Bashir aliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Damascus jana jioni na kulakiwa na mwenyeji wake Rais Bashar al-Assad wa Syria. 

Duru rasmi za habari za Syria zimeripoti kuwa, viongozi hao walijadili na kubadilishana mawazo juu ya uhusiano wa pande mbili pamoja na matukio na migogoro ambayo imezikumba nchi nyingi za Kiarabu.

Katika mazungumzo yao hayo, marais wa Syria na Sudan wamesisitizia udharura wa nchi zao kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na kuchukua hatua za pamoja za kutatua migogoro iliyopo, sambamba na kuheshimiwa mamlaka ya utawala wa ardhi yote katika nchi hizo.

Katika mazungumzo hayo, Rais Assad alimshukuru Rais wa Sudan kwa kuitembelea Syria, na kusisitiza kuwa safari hiyo itatoa msukumo mkubwa wa kurejeshwa uhusiano baina ya nchi mbili katika hali iliyokuwepo kabla ya kuzuka vita nchini Syria.

Rais Omar al-Bashir wa Sudan (kulia) na mwenyeji wake Rais Bashar al-Assad wa Syria (kushoto) baada ya kulakiwa 

Kwa upande wa Rais wa Sudan, mbali na kuashiria kuwa Syria iko mstari wa mbele katika kupambana na magaidi na kwamba kuidhoofisha nchi hiyo si kwa manufaa ya nchi za eneo, Al-Baashir amesema, ana matumaini Damascus itaweza kuchukua tena nafasi muhimu iliyokuwa nayo hapo kabla katika eneo la Mashariki ya Kati haraka iwezekanavyo.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Oktoba mwaka huu, Rais Bashar al-Assad wa Syria alisema katika mahojiano na gazeti moja linalochapishwa nchini Kuwait kuwa, nchi yake imefikia "maelewano makubwa" na nchi za Kiarabu baada ya uhasama wa miaka kadhaa ulioanzishwa na nchi hizo dhidi ya Damascus.../

Tags

Maoni