Dec 17, 2018 15:20 UTC
  • Mawaziri sita wa serikali ya Israel washiriki katika maandamano ya kupinga serikali

Baada ya kupata kipigo kutoka kwa wanamapambano wa Palestina na kulazimika Israel kukomesha uvamizi wake wa Ghaza baada ya siku mbili tu, sasa hivi utawala wa Kizayuni umekumbwa na maandamano ya kuipinga serikali huku mawaziri sita wa serikali hiyo nayo wakishiriki kwenye maandamano ya jana usiku ya kumpinga waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, mamia ya Wazayuni jana usiku waliandamana kwenye makao ya Benjamin Netanyahu kulalalamikia hali ya usalama katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Barabara kuu za Baytul Muqaddas zilifungwa na waandamanaji hao wakitaka kudhaminiwa usalama wao wakiitaka serikali ya Netayahu itume wanajeshi zaidi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Baadhi ya waandamanaji waliokusanyika nje ya makazi ya Benjamin Netanyahu mjini Quds kupinga siasa zake. Mawaziri sita yaani nusu ya baraza lake la mawaziri wameshiriki maandamano hayo ya kumpinga Netanyahu

 

Mawaziri sita wa serikali akiwemo waziri wa elimu, Naftali Bennett, waziri wa mahakama, Ayelet Shaked, waziri wa ujenzi, Yoav Galant na waziri wa kilimo, Uri Ariel wameshiriki kwenye maandamano hayo ya kumpinga Netanyahu.

Kutokana na kupata moyo zaidi baada ya Wazayuni kushindwa vibaya katika vita vya siku mbili huko Ghaza, wanamuqawama wa Kipalestina wamefanya operesheni kadhaa hivi karibuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan licha ya kwamba eneo hilo liko chini ya ulinzi mkubwa wa vikosi vya kijasusi, kijeshi na kiusalama vya Israel.

Wazayuni kadhaa wamengamizwa na kujeruhiwa katika operesheni za hivi karibuni za wanamapambano wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Tags

Maoni