Dec 18, 2018 11:27 UTC
  • Kukiuka Saudi Arabia makubaliano ya Sweden

Baada ya kupita siku tano tangu kufikiwa makubaliano baina ya makundi ya Yemen, Saudi Arabia imeendelea kukiuka makubaliano hayo.

Mazungumzo baina ya makundi ya Yemen yalifanyika tarehe 6 hadi 13 mwezi huu wa Disemba huko Stockholm nchini Sweden chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa Martin Griffiths, mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen ni kuwa, moja ya nukta muhimu na kuu iliyofikiwa na makundi ya Yemen katika mazungumzo hayo ni usitishaji vita katika bandari ya al-Hudaydah, kuwekwa askari huru katika bandari hiyo na kufunguliwa bandari hiyo kwa ajili ya kuingizwa misaada ya kibinadamu.

Pamoja na hayo, ulipita muda wa masaa 24 tu tangu kufikiwa makubaliano hayo wakati muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia ulipofanya mashambulio mara 21 dhidi ya bandari ya al-Hudaydah na kukiuka makubaliano hayo ya usitishaji vita ambayo yameanza kutekelezwa alfajiri ya leo Jumanne.

Makubaliano ya amani ya Yemen,

Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen ametangaza kuwa, juzi tarehe 16 Disemba, ndege za kijeshi za Saudi Arabia zilifanya mashambulio mara 21 dhidi ya bandari al-Hudaydah na mara 26 katika maeneo mengine ya nchi hiyo. Hatua ya Saudia ya kukiuka makubaliano ya amani ya Sweden kuhusu Yemen imeweka wazi nukta hii kwamba, tangazo la Riyadh la kupokea kwa mikono miwili mazungumzo hayo ya Stockholm nchini Sweden halikuwa na ukweli na nia ya dhati, bali ulikuwa ni mchezo wa kisiasa.

Saudi Arabia kwa wiki kadhaa sasa ipo chini ya mashinikizo makubwa kieneo na kimataifa kutokana na kumuua kikatili Jamal Khashoggi na jinai zake dhidi ya wananchi wa Yemen. Mashinikizo hayo ni makubwa mno kiasi kwamba, baadhi ya nchi za Ulaya kama Ujerumani, Finland na Ubelgiji zimesitisha kuiuzia silaha Riyadh huku maseneta wa Marekani wakipasisha azimio lililomtangaza wazi Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia kwamba, ndiye mhusika mkuu wa mauaji ya Khashoggi.

Katika anga na mazingira kama haya, utawala wa Aal Saud usingeweza kuzuia mazungumzo ya makundi ya Yemen huko Stockholm Sweden.  Ni kwa muktadha huo, ndio maana kwa hatua yake ya kupokea kwa mikono mwili mazungumzo hayo, ilikuwa ikitaka kuonyesha kuwa, imechukua mkondo na utendaji mpya kuhusiana na kadhia ya Yemen. 

Mashambulio ya Saudia huko Yemen yanavyoibomoa na kuiharibu Yemen

Ukweli wa mambo ni kuwa, Saudia kwa kujificha nyuma ya wenzo wa mazungumzo inataka kwa namna fulani kutumia njama hii kujionyesha kwamba, inaunga mkono amani na mazungumzo. Hata hivyo, hatua yake ya kukiuka makubaliano hayo na kuendelea kuyashambulia kwa mabomu maeneo mbalimbali ya Yemen imeweka wazi ukweli huu kwamba, hatua yake ya awali ya kutangaza kukarabisha mazungumzo ya amani ya Wayamen ilikuwa mbinu yake ya kisiasa na ya muda iliyolenga kujipunguzia mashinikizo ya kimataifa dhidi yake.

Nukta nyingine ni hii kwamba, utawala wa Aal Saud unaona kuwa, kufanikiwa mazungumzo ya amani ya Stockholm, Sweden ni kushindwa kwake maradufu nchini Yemen. Katika upande mwingine vita nchini Yemen havijawa na natija mwafaka kwa Saudia. Harakati ya Muqawama ya Ansarullah, wananchi na jeshi la Yemen vimeifanya Saudia ipate pigo jingine katika vita vyake dhidi ya nchi masikini zaidi ya Kiarabu ya Yemen.

Tags

Maoni