Jan 16, 2019 16:15 UTC
  • Palestina yakabidhiwa uenyekiti wa kundi la G77, Marekani yapinga

Palestina imekabidhiwa uenyekiti wa kundi la nchi 77 yaani G-77 licha ya Marekani kupinga vikali uamuzi huo.

Akizungumza katika mkutano ambao umehudhuriwa na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahamoud Abbas, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres mbali na kuipongeza Palestina ametoa wito kwa nchi zote kuongeza nguvu kupambana na changamoto zinazoukumba ulimwengu.

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema, taifa lake limepata heshima ya kuchukua uenyekiti wa kundi la 77 na kuongeza kuwa: “Ninayo heshima kwa niaba ya watu wa Palestina na taifa la Palestina kuchukua uenyekiti wa G77 kutoka kwa China kwa mwaka 2019. Hapana shaka ni wajibu mkubwa ambao Palestina itautekeleza kwa utu, kuwajibika na kujitolea kulinda maslahi ya kundi hili na kuimarisha nafasi za wanachama katika Umoja wa Mataifa.”

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Fernanda Espinosa amesema, “Huu ni wakati wa kihistoria na njia tuliyopita kufika hapa haikuwa rahisi. Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa umefanya kazi ngumu, kuanzia katika uamuzi wa kuitoa Palestina katika kuwa mwanachama mwangalizi asiyepiga kura uamuzi uliofanyika mwaka 2012 hadi  uamuzi wa mwaka jana Oktoba wa kuifanya Palestina  kushika nafasi ya urais”

Uenyekiti wa kundi hilo lenye idadi kubwa zaidi ya wanachama ndani ya Umoja wa Mataifa, unazunguka baina ya mataifa wanachama kutoka Afrika, Asia-Pasifiki, Amerika ya Kusini na Karibea na hudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja. Kabla ya Palestina, uenyekiti huo ulikuwa unashikiliwa na China.

Kupitia kundi hilo, nchi hizo za kusini zinachagiza maslahi yao ya kiuchumi na uwezo wa mashauriano kwenye masuala nyeti ya kimataifa ndani ya Umoja wa Mataifa na huchagiza pia ushirikiano baina yao.

Kundi la nchi 77 lilianzishwa tarehe 15 mwezi Juni mwaka 1964 na mataifa 77 kutoka nchi zinazoendelea ambazo zilitia saini azimio la pamoja la nchi 77 zinazostawi.

Tags

Maoni