Jan 24, 2019 08:21 UTC
  • HAMAS: Mpango wa Muamala wa Karne unazilenga nchi zote za Kiarabu na Kiislamu

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, imesema kuwa mpango wa Marekani unaoitwa Muamala wa Karne si tu kwamba unaikusudia Palestina, bali unazilenga nchi zote za Kiarabu na Kiislamu.

Khalil al-Hayya, mjumbe wa ngazi ya juu wa harakati hiyo ya Kiislamu, sambamba na kusisitiza kwamba Ukanda wa Gaza sio tonge tamu kwa ajili ya utawala haramu wa Kizayuni na washirika wake, amesema kuwa muqawama wa Palestina kamwe hautowaruhusu wavamizi ambao mikono yao imetapakaa damu za Wapalestina wafikie ushindi. Al-Hayya ameashiria kuendelea maandamano ya haki ya kurejea na uungaji mkono kwa maandamano hayo na kusema, baada ya Marekani na utawala haramu wa Israel kushuhudia muqawama wa Wapalestina katika kukabiliana na mpango wa Muamala wa Karne zimezidisha mwenendo wa kuboresha uhusiano na nchi za Kiarabu pamoja na utawala wa Kizayuni.

Khalil al-Hayya, mjumbe wa ngazi ya juu wa harakati ya Hamas

Mwaka uliopita 2018 Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza mpango huo kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni. Mpango huo ulio dhidi ya Palestina unaijumuisha Quds na miji yake yote iliyopo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na utawala bandia wa Israel unapinga kikamilifu haki ya kurejea Wapalestina katika ardhi zao za jadi zilizoporwa na utawala huo wa Kizayuni. Aidha mpango huo unalitambua eneo la Abu Dis kuwa mji mkuu wa Palestina. Hata hivyo mpango huo umepelekea kuibuka mizozo na mapigano katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Maoni