Feb 17, 2019 13:56 UTC
  •  Wayemen waandamana kulaani 'Waarabu Wasaliti'

Makumi ya maelefu ya watu wa Yemen wameanadamana kote katika nchi hiyo kulaani nchi za Kiarabu ambazo zinatekeleza usaliti kwa kuanzisha mchakato wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Maandamano hayo yamefanyika katika mji mkuu Sana'a na pia katika mikoa ya magharibi mwa nchi hiyo ya Sa’ada, al-Hudeydah, Ta’izz, na al-Jawf kati ya maeneo mengine.

Kwa mujibu wa Televisheni ya Al Masirah, waandamanaji waliokuwa na hasira wamekosoa vikali kongamano lililoongozwa na Marekani hivi karibuni katika mji mkuu wa Poland, Warsaw. Katika mkutano huo, vongozi na wawakilishi wa ngazi za juu wa nchi kadhaa za Kiarabu walikutana na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala Haramu wa Israel.

Ofisi ya Nyetanyahu imevujisha ukanda wa video kuhusu mikutano ya faragha baina yake na maafisa wa ngazi za juu wa tawala za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi. Washiriki wa mikutano hiyo walitetea ukandamizaji unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina wanaopigania ukombozi huku wakiitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa eti ni tishio.

Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah Sayyid Abdul Malik al Houthi

Waandamanaji nchini Yemen wamewataja watawala wa nchi za Kiarabu wanaojikurubisha kwa utawala haramu wa Israel kuwa ni wasaliti.

Maandamano hayo ya leo nchini Yemen yameitishwa na kiongozi wa Harakati ya Ansarullah Sayyid Abdul Malik al Houthi ambaye ameutaja mkutano wa Warsaw kuwa hatua ya wazi dhidi ya Umma wa Kiislamu.

Maandamano hayo yamefanyika katika hali ambayo, Saudi Arabia, ambayo ni kinara wa tawala za Kiarabu zinazotaka uhusiano wa karibu na Israel, ilianzisha hujuma dhidi ya Yemen mnamo Machi 2015 ambapo hadi sasa maelfu ya Wayemen wasio na hatua wameuawa na mamilioni wanakabiliwa na njaa.

 

Tags

Maoni