Feb 20, 2019 08:06 UTC
  • Hamas: Kujiuzulu kamanda wa makomandoo wa Israel ni ishara ya nguvu ya Wapalestina

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kujiuzulu kamanda wa vikosi maalumu vya makomandoo wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kushindwa na Wapalestina katika oparesheni ya Khan Yunus ni ishara ya nguvu kubwa za harakati za kupigania ukombozi Palestina au muqawama na kusambaratika mahesabu ya wakuu wa utawala wa Kizayuni.

Katika taarifa Jumanne, Hazim Qasim Msemaji wa Hamas alisema: "Kujiuzulu Kamanda wa vikosi maalumu vya makomandoo wa jeshi la utawala wa Kizayuni ni muendelezo wa mtikisiko wa kisiasa katika utawala huo ambao ulianza kwa kujiuzulu Avigdor Lieberman waziri wa vita wa utawala wa Israel jambo ambalo lilipelekea kusambaratika baraza la mawaziri la Kizayuni."

Msemaji wa Hamas ameongeza kuwa, pamoja na kuwepo tafauti kubwa kati ya uwezo wa kijeshi wa harakati za kupigania ukombozi au muqawama na jeshi la Israel, lakini wapigania ukombozi wa Palestina wana imani na wanapigania haki na jambo hilo limepelekea waendelee kuwashinda Wazayuni.

Mpiganaji wa Brigedi za Izzudin Qassam tawi la kijeshi la Hamas

Kamanda wa vikosi maalumu vya makomandoo wa utawala wa Israel alijiuzulu jana baada ya kushindwa vibaya katika oparesheni ya miezi miwili iliyopita huko Khan Yunus kusini mwa ukanda wa Ghaza. Itakumbukwa kuwa, katika oparesheni hiyo ya mwezi Novemba, makombandoo wa utawala wa Israeli walihujumu eneo la Khan Yunus na kumuua shahidi kamanda wa ngazi za juu wa Brigedi za Izzudin Qassam, tawi la kijeshi la Hamas. 

Katika mapigano yaliyofuata, wapiganaji wa Hamas waliwaangamiza na kuwajeruhi makumi ya makomandoo wa Israel. Aidha punde baada ya tukio hilo, kikosi cha makombora cha Hamas kilivurumisha zaidi ya maroketi 500 katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ambapo ngao ya makombora ya utawala wa Israeli inayojulikana kama  'Kuba la Chuma' ilishindwa kuzuia maroketi hayo.

Tags

Maoni