Mar 18, 2019 07:13 UTC
  • Jeshi la Yemen lawaangamiza askari 40 wa Saudia na Sudan mpakani mwa Saudia

Vikosi vya jeshi la Yemen vimewaua askari wanaokaribia 40 wa Saudi Arabia na Sudan katika operesheni mbili tofauti za mashambulio vilizofanya katika eneo la mpaka wa kusini magharibi mwa Saudia, likiwa ni jibu kwa hujuma na mashambulio ya kinyama yanayoendelea kufanywa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Riyadh dhidi ya Yemen.

Msemaji wa Vikosi vya Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema, askari wasiopungua 11 wa Saudia na 26 wa Sudan wameuliwa katika maeneo ya Jizan na Najran.

Kwa mujibu wa Jenerali Saree, katika operesheni hizo, vikosi vya jeshi la Yemen vimezilenga ngome za jeshi katika maeneo hayo baada ya kukusanya na kuhakiki taarifa za kiintelijensia.

Msemaji wa jeshi la Yemen ameongeza kuwa, wanamgambo mamluki wa Saudi Arabia wamepata pigo kubwa pia baada ya askari wa Yemen na wapiganaji wa vikosi vya kujitolea vya wananchi kuzima mashambulio yaliyofanywa katika baadhi ya sehemu za mikoa ya Hudaydah na al-Rabuah.

Wapiganaji wa harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah

Saudi Arabia, ikishirikiana na waitifaki wake kadhaa wa eneo, ilianzisha vita dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuurejesha madarakani utawala kibaraka na tiifu kwa Riyadh. Sudan imechangia askari wake katika uvamizi huo wa kijeshi dhidi ya Yemen.

Nchi kadhaa za Magharibi, hususan Marekani na Uingereza zinaupatia muungano huo vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia silaha na zana za kisasa za kijeshi pamoja na misaada ya kilojistiki na kiintelijensia.

Hadi sasa maelefu ya raia wa Yemen wameuliwa na maelfu ya wengine wamejeruhiwa, mbali na mamilioni wanaotilika kwa maradhi, njaa na kupoteza makazi yao.

Aidha sehemu kubwa ya miundomsingi ya Yemen imeteketezwa, huku mzingiro uliowekwa na Saudia dhidi ya nchi hiyo masikini ukiwakosesha raia maji safi na salama ya kunywa, chakula na huduma za afya.../

Maoni