Mar 19, 2019 15:03 UTC
  • UN: Mauaji ya Wazayuni dhidi ya wakazi wa Ghaza yanaweza kuwa ni jinai za kivita

Operesheni ya Umoja wa Mataifa ya kubaini ukweli imesema kuwa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walivunja haki za binadamu katika ukandamizaji waliowafanyia waandamanaji wa Kipalestina kwenye Ukanda wa Ghaza mwaka jana na ukandamizaji huo unaweza kuhesabiwa kuwa ni jinai ya kivita. Umoja wa Mataifa umeitaka utawala wa Kizayuni uwapige marufuku wanajeshi wake kuwatungua kwa risasi wananchi wa Palestina wanaoandamana kwa amani.

Kamisheni Huru ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ambayo imefanya uchunguzi kuhusiana na maandamano yanayoendelea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, jana Jumatatu ilitoa ripoti yake kamili na kusema kuwa wanajeshi wa Israel wamekanyaga haki za kimataifa za binadamu kwa kutokana na kutumia risasi hai dhidi ya waandamanaji wa Palestina wasio na silaha.

Hali ya wasiwasi ilizuka katika Ukanda wa Ghaza tarehe 30 Machi 2018, baada ya wananchi wa Palestina kuanzisha mlolongo wa maandamano ya "Haki ya Kurejea" katika mpaka wa Ghaza na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.

Mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza

 

Ukatili mkubwa zaidi ulifanywa na wanajeshi wa Israel tarehe 14 Mei mwaka huo, wakati zilipofikia kileleni kumbukumbu za Siku ya Nakba ya kuanza kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina tangu miaka 70 iliyopita. Siku hiyo rais wa Marekani, Donald Trump aliitumia kuzidi kuonesha chuki na uadui wake kwa Waislamu na hasa Wapaelstina kwa kuuhamishia Quds ubalozi wa nchi yake kutoka Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wapalestina 189 waliuliwa shahidi kwa risasi za wanajeshi katili wa Israel na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika kipindi cha baina ya Machi 30 hadi Disemba 31, 2018.

Hata hivyo jinai hiyo ilizidisha hasira za Wapalestina kiasi kwamba maandamano ya "Haki ya Kurejea" yanaendelea kila Ijumaa hadi hivi sasa katika mpaka wa Ukanda wa Ghaza na maeneo mengine ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambayo yamepachikwa jina bandia la Israel.

Maoni